DAR ES SALAAM.
Jumapili 16 Januari 2022 Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amemtembelea na kumjuilia hali ya maendeleo ya afya ya Mzee Rehan B. Waikela aliyelazwa katika taasisi ya mifupa Muhimbili (Moi) akipatiwa matibabu.
“Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake kinathamini na kujali kila mtu aliyejitoa na kujitolea kwa hali, mali, vitu, ujuzi na maarifa kufanikisha uhuru wa Nchi yetu na ukombozi wa Afrika. Mchango wao haupimiki wala hauwezi kuthaminishwa kwa chochote bali kwa kuwatambua, kuwajali na kuwatunza inaweza kuwa namna bora zaidi ya kutambua mchango wao.” Alisema Shaka.
Mzee Waikela amekuwa moja kati ya viongozi wa Chama cha TANU wakati huo ambaye alijitoa na kujitolea kwa hali na mali kuwapa ushirikiano wapigania Uhuru ili kufanikisha lengo hilo.
Historia inamtaja kuwa wakati viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walipokuwa wakifika mkoani Tabora Mzee Waikela alikuwa akiwalaki kwa malazi, chakula na kuwapa huduma ya usafiri ili kuhamasisha harakati za Uhuru na Ujenzi wa Chama cha TANU wakati huo.