Home LOCAL CAMARTEC YAAGIZWA KUBUNI TEKNOLOJIA RAHISI NA NAFUU

CAMARTEC YAAGIZWA KUBUNI TEKNOLOJIA RAHISI NA NAFUU

Naibu Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amekiagiza Kituo cha zana za Kilimo na Teknolojia vijijini (CAMARTEC) kubuni teknolojia  zenye tija kwa gharama nafuu na rahisi kulingana na uwezo wa wakulima na wafugaji nchini bila kuathiri ubora wa teknolojia hizo  ili kufikia malengo ya Taifa kuwa nchi yenye maendeleo ya kiteknolojia na uchumi wa kati-juu ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya 11 ya Kituo hicho, chenye lengo la kukuza matumizi ya zana za kilimo na teknolojia sahihi za vijijini ili kuongeza uzalishaji katika kilimo na kuboresha hali ya maisha ya wananchi vijijini, uliofanyika katika ofisi za CAMARTEC – Arusha.
 
Akizindua Bodi hiyo, Mhe. Kigahe alisema Bodi hiyo ina jukumu la kuandaa Mipango na Mikakati mipya ya kuendeleza Kituo hicho ili kukiwezesha kutoa mchango wake kwa uhakika katika kutekeleza msimamo na mtazamo wa Serikali katika kuendeleza Viwanda na kukuza uchumi wa nchi kwa kuwezesha upatikanaji wa malighafi zinazotokana na uendelezaji Kilimo.
 
“Bodi mnalo jukumu kubwa la kutengeneza mkakati wenu wa kuhakikisha kwamba, malengo ya Taasisi yanafikiwa kwa kusimamia utekelezaji wa mipango yote ya Taasisi. Aidha, katika hili Bodi na Menejimenti mtapimwa kupitia Mkataba wa Utendaji Kazi (Performance Contract) ambao mtausaini Wajumbe wa Bodi, kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi, na Msajili wa Hazina.” Amesema Mhe. Kigahe.

Aidha, Mhe. Kigahe amesisitiza uwepo wa mahusiano mazuri na yenye tija na ushirikiano kati ya Bodi, Menejimenti na Serikali na kuhakikisha kuwa vhombo vyote vitatu vinafanya kazi kama timu muda wote. Pia aliasa Bodi na menejimenti ya CAMARTEC kufanya uchambuzi wakina kuhusu miradi wanayotaka kuitekeleza kabla ya kuiwasilisha na kuhakikisha usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.
 
Pia naibu Waziri na wajumbe wa bodi walipata fursa ya kutembelea karakana za CAMARTEC na kujionea mwenyewe ubunifu wa teknolojia mbalimbali unaofanywa na  kuahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Kituo hicho katika kuhakikisha kuwa Vitovu vya Teknolojia za Kihandisi vinaanzishwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yana uhitaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ambayo ni malighafi muhimu sana ya viwanda vingi nchini vinavyochangia kuongeza wigo wa ajira kwa vijana na akina mama nchini.

 
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwanda  Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara,akimukaribisha Naibu Waziri kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo aliwashauri wajumbe hao kufanya kazi kwa pamoja na Wizara ili kuiwezesha CAMARTEC kusaidia jitihada mbalimbali katika kuboresha mnyororo wa thamani na kuuza mazao yaliyoongezewa Thamani.  
 
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CAMARTEC iliyozinduliwa, Prof. Valerian C. K. Silayo aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na kuifanya CAMARTEC kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kusaidia wakulima ili kuongeza uzalishaji katika kilimo na kuboresha hali ya maisha ya wananchi vijijini.
 
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Kituo kwa Naibu Waziri na wajumbe wa Bodi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC, Bw. Pythias M. Ntella alisema kwa mujibu wa Sheria CAMARTEC inafanya utafiti unaozingatia mahitaji ya wadau inatoa mafunzo na kuhawilisha zana za kilimo na teknolojia za vijijini na inafanya majaribio na kuthibitisha ubora wa zana za kilimo na teknolojia sahihi za vijijini

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here