Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mlimani City Jijini humo ili kuweza kukutana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambao wameweka Kambi kwenye viwanja hivyo kusikiliza na kutatua changamoto zinazoikabili wafanyabiashara.
Afisa Leseni wa BRERA Sada Kilabula ameyasema hayo leo Januari 25,2022 wakati alipozungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku ya kwanza ya Kambi hiyo.
Amesema kuwa BRELA itakuwa hapo kwa siku tano kuanzia leo Januari 26 na kufikia tamati Januari 30 siku ya jumapili mwaka huu.
“BRELA tuko hapa kwa siku tano kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi na kuzipatia ufumbuzi na kuwasaidia kufanya usajili wa Biashara zao pia” Amesema Sada.
Aidha ameongeza kuwa katika Kambi hiyo watatoa fursa ya kuwasaidia wananchi kufahamu jinsi ya kutumia mifumo ya kielektonic itakayowasaidia kupata taarifa mbalimbali za Wakala na kufanya usajili kwa njia ya mtandao.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliofika viwanjani hapo kupata huduma wameishukuru BRELA kuwasogezea huduma na kwamba itawasaidia kupata taarifa sahihi na kupata huduma zote kwa wakati mmoja.
“Uwepo wa BRELA hapa kumenipa fursa ya kufanikisha kurekebisha taarifa za Kampuni yetu, imetusaidia sana kwani imetuokolea muda na imerahisisha sana” Ameeleza Frank Mambali.
Nae Mjasiriamali Marco Luwena ameipongeza BRELA kwa ubunifu mkubwa walioufanya wa kusogeza huduma zao kwa wananchi na kutoa wito kwa wananchi kuitumia vema fursa hiyo.
“Kwakweli huu ni ubunifu mkubwa sana tunapaswa kuwapongeza na kuwashukuru sana BRELA kutupa fursa hii” Amesema Marco.
Uwepo wa Kambi hiyo ya siku tano inatoa fursa kwa BRELA kutekeleza majukumu yake kwa wananchi yakiwemo, Usajili wa Makampuni, Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa hataza, Utoaji wa Leseni za Viwanda, Huduma za Baada ya Usajili na kupata Leseni, na Huduma za kupata taarifa kwa Mtandao.
Mwisho.