Home LOCAL WAUGUZI WASIMAMISHWA KAZI KWA KUFANYA MAPENZI WODINI

WAUGUZI WASIMAMISHWA KAZI KWA KUFANYA MAPENZI WODINI

Picha ya maktaba, MKUU wa wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Paul Chacha

Na: Lucas Raphael,Tabora

MKUU wa wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Paul Chacha amewasimamisha kazi watumishi wawili wa Kituo cha Afya Kaliua kwa tuhuma za kufanya mapenzi wodini wakiwa zamu usiku.

Akitoa taarifa hiyo juzi mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa amechukua hatua hiyo baada ya watumishi hao kulalamikiwa na wagonjwa juu ya kujihusisha na vitendo hivyo wanapokuwa zamu usiku.

Alisema baada ya kupata malalamiko hayo aliitisha kikao cha dharura cha watumishi wote ili kujua ukweli juu ya watumishi hao ambao ni Muuguzi wa kike (Mwajiriwa) na Mganga aliyeko Mafunzoni (sio Mwajiriwa) waliokuwa wakituhumiwa kufanya mapenzi wodini usiku.

Alisema baada ya kujiridhisha kuwepo tuhuma hizo ameamua kuchukua hatua ya awali ya kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi na hatua nyingine za kinidhamu ziweze kuchukuliwa na Mamlaka husika.

Alibainisha kuwa kitendo hicho ni cha utovu wa nidhamu, Mtumishi yeyote wa umma na hata sekta binafsi anapaswa kujiheshimu na kutekeleza wajibu wake kwa kufuata taratibu na miongozo ya kazi yake.

‘Siwezi kufumbia macho tabia za namna hiyo, tutaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mtumishi yeyote asiyezingatia maadili ya utumishi katika eneo lake, huyu mmoja ni Daktari mwanafunzi, anajifunza nini sasa kama anaweza kufanya mapenzi wodini?’alihoji.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amemsimamisha kazi mara moja Mganga wa hospitali ya wilaya hiyo Dkt Irene Apina kwa tuhuma za kukataa  kumpatia matibabu mtoto wa miaka tano na kusababisha kifo chake.

Alisema kuwa kitendo cha Mtumishi huyo kushindwa kumhudumia mtoto huyo kutokana na wazazi wake kukosa fedha za matibabu sio cha kiungwana, alipaswa kumhudumia kwanza ili kuokoa maisha yake.

Aidha Mkuu huyo pia amemsimamisha kazi Muuguzi wa Kituo cha Afya Kaliua Elias Bwire kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utoaji mimba na Muuguzi mwenzake Austina Justin kwa kukiuka maadili ya kazi yake.

Akifafanua juu ya tuhuma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Jerry Mwaga alithibitisha kupokea tuhuma hizo na kubainisha kuwa watazifanyia uchunguzi wa kina na hatua stahiki zitachukuliwa kwa yeyote atakayethibika kuhusika.

Aliongeza kuwa kwa Mtumishi aliyekuwa mafunzoni hayupo tena huku akibainisha kuwa hakuwa mafunzoni bali aliletwa na Shirika moja (jina tunalo) ambao ni wadau wa afya kwa ajili kusaidia kutoa huduma za utabibu.

Wakati huo huo baada ya kupata taarifa za Mganga wa Hospitali aliyekataa kumhudumia mgonjwa (mtoto wa miaka 5) kwa sababu ya kukosa fedha na kusababisha kifo chake, Mkuu wa Mkoa huo Dkt Batilda Burian ameagiza akamatwe na kuwekwa ndani wakati akisuburi hatua nyingine za kinidhamu.

Mwisho.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here