NA:MAELEZO – MBEYA.
Wananchi wa Mkoa wa Mbeya, Halmashauri ya Mbeya Jiji, wamekuwa wakipiga simu kwa watoa huduma ya chanjo kwa ajili ya kupatiwa chanjo ya KORONA katika maeneo yao.
Hayo yameelezwa na Afisa Chanjo wa Jiji la Mbeya, Zuhura Mohamed wakati timu ya Taifa ya Kuhamasisha Njia za Kujikinga na UVIKO-19 Ikiwemo Kupata Chanjo ya KORONA, Awamu ya Pili ilipotembelea Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
“Maeneo mengi ya mjini muitikio ni mkubwa, watu wanapiga simu kuomba kwenda kuchanjwa. Awamu hii ya pili muitikio umekuwa mkubwa tofauti na awamu ya kwanza,” alisema Zuhura.
Aliendelea kusema kuwa, ili kuwarahishia Wananchi kupata huduma ya chanjo waliandika barua iliyoambatana na namba za simu za viongozi wa chanjo wa Jiji ili Wananchi waweze kupiga simu na kupatiwa huduma hiyo kwa haraka, ambapo barua hizo zilibandikwa katika Ofisi zote za Kata za Jiji la Mbeya.
Zuhura aliendelea kusema kuwa, kila Mwananchi aliyepiga simu kwa ajili ya kupatiwa chanjo alifuatwa mpaka eneo alipo na kupatiwa huduma hiyo.
Zoezi la kuhamasisha njia za kujikinga na UVIKO-19 ikiwemo kupata chanjo ya KORONA, awamu ya Pili, linaendelea nchi nzima, ambapo kwa awamu hii, Wananchi wanafuatwa hadi majumbani ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata chanjo na kuwa salama.
Takwimu za Tanzania zinaonyesha kuwa katika kila wagonjwa 10 waliolazwa hospitalini sababu ya UVIKO-19, basi wagonjwa 8 ni wale ambao hawakuchanja na wa 2 ni waliochanja na waliochanjwa ugonjwa wao ni mwepesi zaidi kuliko wasiochanja.
Aidha, kati ya 10 wanaofariki kwa UVIKO-19, basi 7 ni wale wasiochanja na wa 3 ni waliochanja na unakuta bahati mbaya miili yao ilizidiwa kiafya na magonjwa mengine sugu mfano ugonjwa wa kisukari, presha, uzito uliopitiliza, hali ya uzee na magonjwa mengine yote yanayodhoofisha kinga ya mwili.