Home BUSINESS WAKULIMA KALIUA WAPEWA MBINU KUONGEZA UZALISHAJI

WAKULIMA KALIUA WAPEWA MBINU KUONGEZA UZALISHAJI

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Jafael Lufungija akisisitiza jambo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo i, kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Abdallah Hemed na kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga na Ofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Na: Lucas Raphael,Tabora

WAKULIMA wilayani Kaliua Mkoani Tabora wametakiwa kuzingatia matumizi ya kanuni za kilimo bora cha mazao ya chakula na biashara katika msimu huu mpya ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya jamii na taifa kwa ujumla.

Ushauri huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Jafael Lufungija alipokuwa akiongea na madiwani, wataalamu na watendaji wa halmashauri hiyo katika kikao cha baraza.

Alisema wilaya hiyo imejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba inayofaa kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hivyo katika kuhakikisha azma yao inatimizwa wakulima wameendelea kuhamasishwa kuzingatia kanuni za kilimo bora.

Alibainisha baadhi ya kata ambazo elimu hiyo imeshatolewa kuwa ni pamoja na Ilege, Seleli, Kona nne, Sasu, Makingi, Kanoge, Usenye, Usinge, Uyowa, Silambo na nyinginezo.

Mbali na hamasa aliongeza kuwa pia wamefanya mikutano ya usuluhishi kwa baadhi ya vyama vya msingi vinavyojishughulisha na kilimo cha tumbaku ambavyo vimekuwa na migogoro ya muda mrefu ambayo imekuwa ikizorotesha uzalishaji wa zao hilo.

Mwenyekiti alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga kwa kushirikiana na Ofisa Ushirika na Maofisa Ugani walioko katika vijiji kwa kusimamia vizuri wakulima.

Aliongeza kuwa juhudi zao zimesaidia kufufuka kwa baadhi ya vyama vya msingi vilivyokuwa vimekufa katika vijiji vya Usinge na Nsungwa ambavyo ni Usinge na Ntyemo Amcos.

Mkurugenzi Mtendaji, Mwaga, alisema katika kuhakikisha shughuli za wakulima zinaboreshwa wamekutana na wadau wa tumbaku na kufanya tathmini ya masoko na changamoto zilizopo ili kuzitafutia ufumbuzi.

Aliongeza kuwa usimamizi mzuri wa masoko umewezesha kuuzwa kwa kilo mil 8.9 sawa na asilimia 84 ya tumbaku iliyozalishwa mwaka jana na kuingizia wakulima dola za Kimarekani mil 14.5 sawa na sh bil 33.2.

Alibainisha kuwa katika msimu wa 2020/2021 jumla ya kilo 840,530 za pamba zilizalishwa na kuuzwa zote na kuongeza kuwa halmashauri kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti (TARI) Tumbi wameanza mchakato wa kuzalisha mbegu bora za michikichi katika Kijiji cha Usindi.

Aidha aliongeza kuwa wameanzisha ujenzi wa kitalu nyumba (green house) kwa ajili ya kufundishia teknolojia ya kilimo ambapo zaidi ya vijana 100 wanatarajiwa kupata mafunzo kupitia kitalu hicho.

Mwisho.

Previous articleBILIONI 48.5 KUKAMILISHA UJENZI NA KUNUNUA SAMANI ZA VYUO 25 VYA UFUNDI STADI
Next articleRPC AWATUMIA SALAMU WANAOJIHUSISHA NA VITENDO VYA UHALIFU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here