Home LOCAL UJERUMANI YAIPONGEZA TANZANIA MAPAMBANO YA UVIKO-19, YAKABIDHI VIFAA TIBA VYA BILIONI 2

UJERUMANI YAIPONGEZA TANZANIA MAPAMBANO YA UVIKO-19, YAKABIDHI VIFAA TIBA VYA BILIONI 2





DAR ES SALAAM.

Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regina Hess, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi inazochukua kupambana na ugonjwa wa Uviko-19 ambazo zimezaa matunda kufuatia uwepo wa visa vichache vya ugonjwa huo vilivyorekodiwa wimbi lililopita.

Mhe. Hess amesema Serikali ya Ujerumani inaridhishwa na hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Tanzania katika kupamabana na Uviko-19, ikiwemo elimu kwa wananchi pamoja na kampeni ya uhamasishaji ya kuhakikisha watanzania wanapata chanjo ya UVIKO-19

Balozi Regina Hess ametoa pongezi hizo leo 16/12/2021 wakati akikabidhi msaada wa vifaa tiba, vilivyotolewa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la GIZ, kwa Mfamasia Mkuu wa Serikali na Uongozi wa MSD kwenye Makao Makuu ya Bohari ya Dawa (MSD) yaliyoko Keko jijini Dar es salaam.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya takribani shilingi bilioni mbili na laki tatu (2.330.958.072) vikijumuisha mashine za kusaidia kupumua 50 (ventilators)na mashine za kupima kiwango cha Oksjijeni ndani ya mwili zipatazo 5000 (pulse oximeters).

Balozi Hess ameongeza kwamba Serikali ya Ujerumani imekua ikishirikiana na itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye Nyanja mbalimbali za kimaendeleo, ikiwemo sekta ya afya, hasa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19, ambapo awali ilitoa msaada wa maabara zinazotembea kwa serikali ya Tanzania ili kurahisisha upimaji wa wagonjwa wa UVIKO-19.

Akipokea Vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali, Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi, ameishukuru Ujerumani kwa kuendelea kusaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, na kusema vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Ujerumani kwani msaada huu umekuja kwa wakati muafaka, hasa kipindi hiki ambacho dunia imeshuhudia mlipuko wa wimbi jipya la virusi vya Corona aina ya Omicron tutasambaza vifaa tiba hivi kwenye maeneo mbalimbali nchini, ili vikaongeze nguvu kwenye mapambano dhidi ya UVIKO-19” alisema Msasi.

Bw.Msasi amesisitiza kwamba Vifaa tiba hivyo vitasambazwa kwenye takribani vituo 500 vya kutolea huduma za afya nchini, huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na Ugonjwa wa UVIKO-19 hasa kipindi hiki cha kuelekea msimu wa sikukuu, kwa kuhakikisha wanavaa barakoa, kuepuka misongano na kuchanja kwa hiari.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Bw. Billy Singano amesema MSD imekwisha pokea vifaa hivyo kwenye maghala yake, na inaendelea na mchakato wa kuvisambaza kuipitia Kanda zake, huku akisisitiza kila kituo kitakachokua kimeainishwa kitapokea mgao wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here