Home LOCAL UCHAGUZI MDOGO NALASI KUFANYIKA JUMAPILI

UCHAGUZI MDOGO NALASI KUFANYIKA JUMAPILI

Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mdogo wa Udiwani kata ya Nalasi Mashariki Jimbo la Tunduru Kusini wakila kiapo cha Utii mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini Chiza Malando(hayupo pichani)wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo katika mchakato wa uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.

Baadhi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura na wasimamizi wasaidizi wakimsikikiliza  Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tunduru Kusini Chiza Malando(hayupo pichani)wakati wa  ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uelewa katika kazi ya kusimamia uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Nalasi Mashariki Jimbo la Tunduru Kusini unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 Mwezi huu.

Na: Muhidin Amri, Tunduru

WASIMAMIZI wasaidizi wa Uchaguzi na makarani waongozaji wapiga kura katika jimbo la Tunduru Kusini wilayani Tunduru ,wametakiwa kujiepusha na itikadi za vyama,badala yake wametakiwa kutenda haki kwa kila chama  na Mgombea wakati  wa mchakato wa uchaguzi ili kuepusha vurugu na malalamiko.

 Msimamizi wa uchaguzi jimbo  la Tunduru Kusini Chiza Malando,alisema hayo jana wakati akifungua mafunzo kwa makarani waongozaji wapiga kura  na wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi  wa vituo vya kupigia kura  katika uchaguzi mdogo wa Udiwani kata ya Nalasi Mashariki.

Uchaguzi huo unatarajia kufanyika mwishoni mwa wiki hii, kufuatia  kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo Mohamed Mlehani aliyefariki Dunia mwezi Septemba mwaka huu.

Malandu amewaasa wasimamizi hao kwenda kutekeleza vema mambo waliofundishwa ikiwemo suala la uadilifu,uaminifu,weledi  na kujiepusha na vitendo vyovyote vinakwenda kinyume na sheria za uchaguzi vinavyoweza kuvuruga uchaguzi huo.

Alisema,uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri,wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa malalamiko au  vurugu wakati wote wa uchaguzi.

Alisema,matumaini ya tume ya uchaguzi kwamba  baada ya kupata mafunzo hayo watakwenda kufanya kazi za tume kwa juhudi,maarifa  ili kufanikisha uchaguzi na kuzingatia maelekezo watakayopewa  na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea na kuhakikisha wanazingatia matakwa ya Katiba,Sheria na kanuni zinazosimamia zoezi la uchaguzi.

Malando ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tunduru  alisema, wakati wote wa mchakato wa uchaguzi  huo,wasimamizi watafanya kazi kwa kufuata maelekezo ya tume na msimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo kwa kushirikiana na vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo na siyo vinginevyo.

Baadhi ya washiriki walisema, mafunzo hayo yamekuwa mazuri kwa sababu yamewapa uelewa katika usimamizi wa zoezi zima la uchaguzi na uzoefu wa kwenda kutekeleza majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lipepo Shaibu Kadewele ameishukuru Halmashauri ya wilaya Tunduru kwa kutoa mafunzo ambayo yatawajengea uwezo na uelewa katika suala zima la majukumu yao ya usimamizi katika uchaguzi mdogo wa udiwani.

Alisema, kimsingi mafunzo hayo yamewapa dira namna ya kwenda kutekeleza  majukumu yao ikiwemo suala la  kushirikiana na vyama vya siasa,wananchi  na namna ya kutumia kanuni na taratibu zilizoainishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
MWISHO

Previous articleKAMPUNI YA TUMBAKU YABORESHA HUDUMA ZA JAMII
Next articleTEA YARIDHISHWA NA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU LINDI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here