Home BUSINESS TMDA YATOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU UDHIBITI WA TUMBAKU RUKWA

TMDA YATOA ELIMU KWA UMMA KUHUSU UDHIBITI WA TUMBAKU RUKWA

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa (kulia) akifurahia jambo leo alipokutana kwa mazungumzo na Kaimu Meneja wa Kanda wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshighati toka Mbeya (kushoto). TMDA wapo Rukwa kutoa elimu kwa umma juu ya athari za tumbaku .


Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa (wa kwanza kulia) akizungumza na Kaimu Meneja wa Kanda wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshighati (katikati) Ofisini kwake Sumbawanga. (Wa kwanza kushoto) ni Afisa Habari na Mahusiano toka TMDA Mbeya Prisca Matagi.

RUKWA. 

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imepongezwa kwa kutoa elimu juu ya matumizi na athari za tumbaku na mazao yake kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa hususan Vijijini.

Pongezi hizo zimetolewa leo (15.12.2021) na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa wakati wa kikao chake na Maafisa wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye makao makuu yake Mbeya waliofika ofisini kwake Sumbawanga  kuelezea  kazi ya uelimishaji umma juu ya majukumu ya TMDA katika udhibiti wa tumbaku kwenye wilaya za Rukwa.

“Ninawapongeza kwa kufika maeneo mengi ya pembezoni huko vijijini ambapo kuna watu wengi na kuwapa elimu juu ya athari za matumizi ya tumbaku kwa afya zao ili wachukue hatua za kufanya maamuzi sahihi” alisema Bandisa

Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliwataka Maafisa hao wa TMDA kujitahidi kufika kwenye maeneo yenye watu wengi zaidi Vijijini na kutoa elimu ya shughuli za Mamlaka hiyo muhimu katika kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya dawa na vifaa tiba ikizingatiwa kuwa mkoa wa Rukwa upo mipakani na nchi za DRC Congo na Zambia

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshighati alieleza kuwa tayari wamefanikiwa kufika katika wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga ambapo wametoa elimu kwa wajumbe wa kamati za maendeleo ya kata nne kila halmashauri.

Mshighati alitaja mafanikio mengine kwenye zoezi hili kuwa wametoa elimu juu ya majukumu ya TMDA na athari za tumbaku kwa vyuo vya Waganga St. Bakita cha Nkasi pamoja na Chuo cha Waganga Sumbawanga.

“Tupo hapa Rukwa tangu Desemba 08 mwaka huu tukitoa elimu kwa umma juu ya madhara ya tumbaku na namna ya kukabiliana nayo ikiwa ni jukumu la Mamlaka yetu TMDA kuelimisha wananchi “alisema Mshighati.

Mtaalam huyo wa dawa alisema katika kazi hiyo wamepata wasaa wa kuongea na wananchi kwenye vikao vya kata nyingi ambapo wamebaini kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu kwa wananchi juu ya athari za matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Wataalam hao wa TMDA pia leo wameshiriki kutoa elimu athari za tumbaku kupitia redio Chemchem FM na Ndingala FM za mjini Sumbawanga ambapo wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali na kujibiwa.

Kesho wataendelea na kazi ya kutoa elimu ya udhibiti tumbaku na mazao yake kwa kamati za maendeleo za kata za Mwadui, Muze, Mkwawa na Ikozi zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here