Rais wa chama cha mawakili Tanzania, Dkt Edward Hoseah akiongea katika mafunzo ya mawakili inayoendelea mkoani Arusha.
Mawakili wakifuatilia jambo katika mafunzo yao yanayoendelea mkoani Arusha.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo wakili Silvia Mwanga akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo wanayotoa kwa mawakili
NA: NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Rais wa chama cha mawakili Tanzania, Dkt Edward Hoseah amempongeza Mkurugenzi mkuu wa mashtaka nchini(DPP) Sylvester Mwakitalu kwa kuondoa mashauri yakiwemo yasiyo na ushahidi mahakamani jambo litakalo saidia kupunguza mrundikano wa kesi.
Akiongea na waandishi wa habari mkoani Arushaleo katika mafunzo ya mawakili Dkt Hoseah alisema DPP amejitahidi kwani amefanikiwa kuondoa mashauri hayo mahakamani ambapo hiyo ni sehemu ya utendaji mzuri wa kazi.
Alisema kuwa ushauri wao kama Mawakili ni kwamba ni vyema wakazingatia kutopeleka kesi mahakamani kama hazina ushahidi kwani hali hiyo itapunguza mrundikano wa mashahuri mahakamani.
“Pamoja na hayo sisi kama Mawakili wiki hii yote tumeanza na anuai za kitaaluma pamoja na kutoa mada mbalimbali ikiwemo sheria zinazohusu utakatishaji fedha pamoja na uhujumu uchumi ikiwa lengo ni kuona ni kwa namna gani sheria zinavyosadifiana na mikataba ya kimataifa,”amesema Prof.Hoseah.
Amesema katika nchi ya Tanzania utakatishaji fedha ni kosa kubwa ambavyo kupitia sheria mtuhumiwa hupewa adhabu hivyo wameweza kujifunza mambo hayo na ikiwa kama wanasheria wanao wajibu wa kutoa taarifa kwa makosa hayo.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo wakili Silvia Mwanga alisema lengo ni kutoa elimu kuhusu sheria ya ukusanyaji kodi na masuala ya utakatishaji fedha ambayo yamekuwa bado ni tatizo kwa upande wa wananchi na baadhi ya wanasheria.
Aidha alisema kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya utakatishaji fedha bado kuna haja ya kuendelea kupewa mafunzo ya kila mara ili kuwa katika nafasi nzuri yakuweza kuyasimamia vyema.
“Tutaendelea kutoa mafunzo yakiwemo masuala ya ndoa ili kusaidia kufahamu sheria zake katika kuwajengea mawakili uwezo ya kuwa kwenye nafasia nzuri katika kusaidia jamii pamoja na mahakama kufikia masuala ya haki kwa kila mtu,”amesema Wakili huyo.