TMDA
Home LOCAL TEA YARIDHISHWA NA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU LINDI

TEA YARIDHISHWA NA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU LINDI

Muonekano wa mradi wa ujenzi wa nyumba nne za waalimu zilizofadhiliwa na Mamlaka ya  Elimu Tanzania (TEA) katika Shule ya Sekondari Kassim Majaliwa iliyopo wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Profesa. Bernadeta Killian (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, walimu wa Shuleya Sekondari Kassim Majaliwa na watendaji kutoka TEA baada ya kupokea taarifa na kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba nne za waalimu kwenye shule hiyo.


Muonekano wa vyumba vitatu vya madarasa vilivyo karabatiwa kupitia ufadhili wa miradi ya elimu chini ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).


Muonekano wa madarasa yaliyokuwa yanatumiwa na wanafunzi katika Shule ya Msingi Mnimbila kabla ya ujenzi wa vyumba vitatu vipya vilivyofadhiliwa na TEA


Ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ukiendelea katika Shule ya Msingi Ngwenya, mradi ambao uliipandisha hadhi shule hiyo kutoka shule ya awali na kuwa shule ya awali na msingi

 Na: Eliafile Solla – TEA.

MIUNDOMBINU bora ya elimu katika Halmashauri nyingi hapa nchini ni changamoto kubwa ambayo haiwezi kuachiwa Serikali peke yake, bali kuna haja ya kuongeza ushirikiano wa jamii katika kutatua changamoto hizo kupitia uchangiaji wa rasilimali fedha au vifaa katika Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Mfuko wa Elimu wa Taifa ulianzishwa kwa Sheria Namba 8 ya mwaka 2001, ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuwezesha maendeleo ya Elimu katika ngazi zote kwa Tanzania Bara na Elimu ya Juu kwa Tanzania Zanzibar. 

Lengo la kuanzishwa Mfuko wa Elimu wa Taifa ni kuongeza nguvu za Serikali katika kugharamia miradi ya elimu, ili kuinua ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa katika mazingira ambayo hayafikiki kiurahisi.

Mkoa wa Lindi ni moja kati ya wanufaika wa miradi ya elimu ambayo inafadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambapo baadhi ya shule zilizopata ufadhili ni shule ya Sekondari Kassim Majaliwa Wilayani Ruangwa iliyopewa ufadhili wa ujenzi wa nyumba nne za waalimu, Shule ya Msingi Ngwenya na Mnimbila Manispaa ya Lindi, ambazo zote zilipata ufadhili wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa.

Katika ziara ya viongozi wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) iliyofanyika wiki hii kwenye miradi hiyo, uongozi wa bodi ulionesha kuridhishwa na hatua ya utekelezaji katika miradi yote baada ya kukuta mingi ikiwa imekamilika kwa wakati na mmoja ukiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji.align: 

Kiongozi wa msafara katika ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TEA Profesa.Bernadeta Killian aliwapongeza waalimu wa shule na viongozi wa Halmashauri zote baada ya kupokea taarifa kuhusu miradi kwenye maeneo yao na kulinganisha taarifa alizopokea na alichokiona uwandani.

“Kwa kweli kazi mnayoifanya inaonekana ukilinganisha na thamani ya kiasi cha fedha mlichopewa na TEA kutoka kwenye Mfuko wa Elimu wa Taifa japo bado kuna uhitaji. Niseme tuu kwamba, Tanzania ni kubwa sana na miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ni changamoto hivyo tuendelee kutumia hizi zilizopo kuongeza ubora wa elimu” alisema Killian.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngwenya, Masaninga Twende alibainisha kwamba, mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya Ngwenya umeipandisha hadhi shule hiyo kutoka shule ya awali hadi kusajiliwa na kuwa shule ya awali na msingi ingawa bado kuna uhitaji wa darasa moja na nyumba za waalimu.

Aliongeza kuwa, kabla ya ujenzi wa vyumba hivyo wanafunzi walikuwa wanaletwa kusoma hapo madarasa ya awali kama njia ya kuwaandaa kutembea kilomita zaidi ya mbili kuendelea na shule ya msingi hivyo kusababisha wengi kushindwa kutembea umbali huo na matokeo yake kuacha shule.

Aidha, Masaninga alisisitiza kwamba, kupatikana kwa vyumba hivyo vya madarasa kumeipa sifa shule hiyo kuwa shule ya msingi na sasa hivi wanafunzi kutoka katika vijiji vya karibu wanapata fursa ya kusoma na kujifunza ambapo kwa mwaka huu wa masomo jumla ya wanafunzi 12 walifanya mtihani wa darasa la saba na wanafunzi 9 kati yao walifaulu na wanatarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwakani. 

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inatekeleza kazi zake chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia huku ikisimamia dhamira ya kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa na kuzigawa rasilimali hizo kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali ili kufadhili miradi ya elimu kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea TEA YARIDHISHWA NA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU LINDI