Home BUSINESS SIDO YAAGIZWA KUJENGA KITUO KIKUBWA CHA TEKNOLOJIA ILI KUONGEZA UZALISHAJI BIDHAA BORA...

SIDO YAAGIZWA KUJENGA KITUO KIKUBWA CHA TEKNOLOJIA ILI KUONGEZA UZALISHAJI BIDHAA BORA KWA WINGI ZINAZOKIDHI MAHITAJI YA SOKO


DODOMA.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaudi Kigahe ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kujenga kituo kikubwa cha kuendeleza Teknolojia (TDC) katika Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kutengeneza bidhaa mbalimbali za mashine zenye ubora kwa wingi  kulingana na soko la ushindani.

Kigahe ameyasema hayo alipokuwa akiongea na menejimenti  na wafanyakazi wa Ofisi ya SIDO Mkoa wa Dodoma alipokuwa akifanya ziara ya kukagua miradi inayosimamiwa na SIDO, Mitaa ya Viwanda na Wajasiliamali wanaowezeshwa na SIDO ili kusilikiza changamoto zao na kuona jinsi Serikali inavyoweza kuzitatua katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Geita na Mwanza kuanzia Novemba 30 hadi Disemba 5, 2021.

Aidha, Naibu Waziri pia ameielekeza SIDO kuandaa mpango wa kupanua wigo wa utoaji wa huduma zake katika Wilaya za kimkakati zenye viwanda vingi na zinazohitaji huduma za SIDO ili kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa za kati ambazo ni malighafi kwa wingi kwa ajili kuzalisha bidhaa za mwisho ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuuza bidhaa hizo kwa bei nafuu.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alitembelea Mitaa ya Viwanda ya SIDO na wajasiliamali wanaonufaika na huduma za SIDO kwa kutumia Mikopo kupitia mifuko ya NEDF na CREDIT GUARANTEE SCHEMES, Maeneo ya kufanya kazi ambapo wanalipa kodi bei nafuu kuliko maeneo mengine, Mafunzo kwa wajasirimiali wakusindika vyakula, mvinyo na watengenezaji wa bidhaa za ngozi na Kuunganishishwa na Taasisi nyingine za Serikali kama BRELA, TBS na GCLA ili kupata vibali vya kuzalisha bidhaa zao, kuzirasimisha na kupata nembo za ubora.


Viwanda vilivyotembelea na Mhe. Kigahe ni pamoja na Mtaa Mdogo wa Viwanda (RO) ulipo katika Ofisi za SIDO Dodoma wenye wapangaji 32 wenye jumla ya Ajira 228. Viwanda hivyo ni pamoja na  kiwanda cha BOSA General Supplies ltd kinachopisha Risiti, Ankara na Nyaraka tofauti kwa ajili ya Halmashauri na Manispaa mbalimbali Tanzania, Watengenezaji wa bidhaa za chuma kama vile Vitanda vya nyumbani na hospitali, Mashine za kufyatulia matofali, Mafundi wanaofanya service za magari na wanashirikiana na Taasisi ya VETA kufundisha vijana wa ufundi wa magari na Umoja wa Mafundi Seremala (UMASE).

Maeneo mengine yaliyotembelewa ni pamoja na Kituo cha Usindikaji Ngozi TPC-KIZOTA kinachotoa mafunzo  ya usindikaji wa ngozi na bidhaa za chakula na kutoa vyeti kwa wahitimu wa usindikaji wa ngozi katika kituo hicho.

Pia  alitembelea Mtaa wa Viwanda SIDO-Kizota ambao hadi sasa una viwanda 9 (Unga-3, Mvinyo-2, Maji-1, Viungo-2 na Alizeti-1) ikiwemo kiwanda cha Home mate food kinachosindika unga wa Sembe, Kamete Investiment kinachotengeneza maji ya kunywa yanayoitwa DODOMA pure Drinking Water na kiwanda cha Robert Paul Winery Co. ltd kinachotengeneza Mvinyo wa aina za Tanport-Red sweet wine na Kampor- Red dry wine.

Aidha, Naibu Waziri aliwatembelea  wajasiliamali wanaohudumiwa na SIDO- Dodoma ambao ni Kiwanda cha Bakel Company Ltd kinachotengeza Mvinyo wa BAREPO (Semi sweet wine) na Saint Gema Bakery Bread kinachomilikiwa na Watawa Wakatoliki wanaotengeneza mikate, keki, maandazi na skonsi.

Wakiongea na Naibu Waziri Wajasiliamali waliotembelewa walieleza changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa upatikanaji wa vifungashio haswa vya mvinyo kwakuwa vifungashio vingi vinaagizwa kutoka nje ya nchi,  Upatikanaji mdogo wa mitaji ya kuendeleza biashara kwa kuwa Mfuko wa NEDF hauna mtaji wakutosha na kima cha juu cha kukopa ni kidogo kulingana na mahitaji ya viwanda na  upatikanaji wa malighafi ya uzalishaji hususani wa mvinyo(wine) ambazo hazipatikani kwa mwaka mzima  na kufanya Viwanda hivyo kutokuzalishwa mvinyo kwa mwaka mzima.

Naye Mkurugenzi wa SIDO Mhandisi Prof. Sylvester Mpanduji akimkaribisha Naibu waziri katika Ofisi za SIDO-Dodoma alieleza kuwa SIDO imeendelea kutekeleza majukumu yake kama ilivyoanishwa katika Sheria ya Bunge na 28 ya mwaka 1973 kwa kutoa huduma za kiufundi na maendeleo ya teknolojia, uanzishaji wa miradi ya viwanda vidogo vijijini, mafunzo, ushauri na huduma za ugani, masoko na habari, na huduma za fedha kwa wajasiliamali wadogo ili kuendeleza sekta ya Viwanda na Biashara na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Akitoa taarifa fupi ya huduma zinazotolewa kwa Naibu Waziri, Kaimu Meneja wa SIDO- Dodoma  Bw. Justice Kahemela  alisema  SIDO – Kanda ya kati inahudumia zaidi ya Wilaya 7 na Halamshauri 8 na  imeainisha fursa mbalimbali zilipo katika kuanzisha viwanda mkoani Dodoma kulingana na  uwepo wa malighafi za kilimo (Zabibu, Alizeti, Karanga),  uwepo wa madini kama (Dhahabu, gypsum), uwepo wa ardhi ya kutosha, miundombinu bora (barabara, maji, umeme), uwepo wa njia za kuunganisha nchi jirani pande zote na Makao Makuu kuhamia Dodoma.

Aidha, Bw. Kahemela alisema SIDO imetenga maeneo matatu yakufanya biashara na kuendeleza wajasiriamali Mkoa wa Dodoma ambayo ni Mtaa Mdogo wa Viwanda (RO), Kituo cha ngozi TPC-KIZOTA, Mtaa wa Viwanda KIZOTA. Pia alisema SIDO inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na taasisi mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here