Wafanyakazi wa shirika hilo Mkoa wa Singida wakiwa kwenye banda lao wakati wa maadhimisho hayo. Kutoka kulia ni Mhandisi wa Mkoa wa Shirika hilo Albert Guruyedi, Mhasibu wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Renalda Mlambo na Afisa Miliki Israel Ngapona,
Na: Dotto Mwaibale,Singida.
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida limejivunia mafanikio yake ya miaka 60 ya Uhuru kutokana na shughuli mbalimbali ilizozifanya katika kipindi hicho.
Hayo yalibainika katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 59 ya muungano yaliyofanyika jana kimkoa katika Wilaya ya Manyoni.
Akielezea mafanikio hayo Mhandisi wa Mkoa wa Shirika hilo Albert Guruyedi alisema Shirika hilo limejenga nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo pamoja na nyumba za biashara kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Nyumba kwa bei nafuu.
“Tunawakaribisha wananchi mje mpange kwenye nyumba za Shirika la nyumba,zipo za makazi na za kibiashara karibuni sana.” alisema Mhandisi Guruyedi.
Alisema wakati wa maadhimisho hayo NHC linajivunia mafanikio makubwa mengi ambayo pia yanaendelea kupatikana kwa maslahi sio tu ya shirika la nyumba bali na kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Singida.
Alisema shirika hilo wametumia fursa ya maadhisho hayo kutangaza nafasi walizonazo za majengo ya biashara mawili ya ambayo yamebaki na nafasi chache.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge alilipongeza Shirika hilo kwa mafanikio hayo na kulitaka kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokuwa inakusudiwa na Serikali wakati inaanzisha shirika hilo hapa nchini.
Alisema shirika la nyumba limechangia mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Miaka 60 ya Uhuru katika sekta mbalimbali ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa nyumba za kupangisha kwa bei nafuu.
Mkoa wa Singida umeadhimisha siku ya miaka 60 ya uhuru kwa takribani siku nne kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria,kufanya kongamano,michezo na baadaye kuhitimishwa kwa hutuba mbalimbali za viongozi.