Na: stella Kessy, DAR ES SALAAM.
SERIKALI kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limewapongeza waogeleaji na makocha wao kupitia Chama cha Taifa Mchezo huo (TSA) kwa kuipeperusha vyema Bendera ya nchi katika mashindano ya Afrika kanda ya 3.
Kauli hiyo imesemwa na leo Disemba 12, Uwanja wa ndege wa Mwl. Nyerere na Halima Bushiri Afisa Michezo wa BMT kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo wakati akiwapokea waogeleaji hao 23 walioiwakilisha nchi katika michuano ya Afrika kanda ya 3 yaliyomalizika tarehe 11 Disemba, 2021 nchini Uganda.
Halima aliendelea kwa kuwahakishia Viongozi wa chama na wazazi waliofika kuwapokea watoto wao kuwa Serikali ipo pamoja nao na kutoa wito kwa wazazi na makampuni kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na chama pamoja na wanamichezo.
Mashindano hayo yalishirikisha nchi sita (6) za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Eritrea, Burundi Rwanda, Sudan na mwenyeji Uganda.
Timu ya Tanzania imeibuka na ushindi wa pili wa jumla baada ya kuchukua ushindi wa tatu jumla kwa wanawake, mshindi wa pili wa jumla kwa wanaume, na ushindi wa wa makundi, umri wa miaka 12 kwenda chini jinsia zote imeibuka na ushindi wa kwanza kwa kutoa wachezaji bora wawili Austin Okele na Filbertha Demello wanawake.
Kundi la Miaka 13 -14 timu ya Tanzania imetoa mchezaji bora kwa upande wa wanawake Sophia Latiff, 15 -16 ametoka mshindi wa kwanza ambaye ni Ria Save, kundi la miaka 17 nakuendea Tz imetoa mchezaji bora Collins Saliboko.
Awali akizungumza na vyombo vya habari kabla ya kutoka kwa waogeleaji hao ndani ya Uwanja wa ndege wa Mwl.Nyerere kocha Mkuu Maiko ameeleza kuwa, ushindi huo unawapelekea waogeleaji wao kupata vigezo vya kushiriki katika mashindano ya ngazi ya juu zaidi.
Naye Nahodha wa timu hiyo Collins Saliboko ameeleza kuwa ushindi wao umetokana na mazoezi ya muda mrefu pamoja dua za Watanzania.
Wachezaji hao waliagwa na kukabidhiwa bendera na Naibu Waziri mwenye dhamana ya michezo Mhe. Pauline Gekul akiwataka kurudi na ushindi.