– Ni fedha Asilimia 10 Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu.
– Ampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia fedha Za mikopo kutengwa.
N: James Lyatuu, DAR ES SALAAM.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla leo amekabidhi hundi ya Shilingi Bilioni 2 kwa vikundi *97* vya Kujikwamua kiuchumi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya Asilimia 10 ya Mapato ya ndani ambayo hutengwa kwaajili ya Mkopo wa kuwaendeleza Wanawake, Vijana na Watu Wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa Hafla ya kukabidhi hundi iliyoambatana na Maonyesho ya wajasiriamali Viwanja vya Mnazi mmoja, RC Makalla amepongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kwa kutekeleza agizo la Serikali la kuwezesha Wananchi kiuchumi.
Aidha RC Makalla amevitaka vikundi vinavyokopeshwa kurejesha Fedha za Mkopo kwa wakati ili fedha hizo ziweze kusaidia vikundi Vingine.
Hata hivyo RC Makalla amezielekeza Manispaa nyingine za Mkoa huo kutekeleza takwa la kisheria kwa kutoa Asilimia 10 ya Mapato ya ndani kuviwezesha vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye ulemavu.
RC Makalla pia ametoa wito kwa Wananchi kununua bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wazawa ili kuinua uchumi wa Taifa na kutoa wito kwa wajasiriamali kuwa wabunifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Jumanne Shauri amesema katika Bilion 2 zilizotolewa, vikundi 46 vya Wanawake vimepata Milion 980, Vikundi 43 vya Vijana Shilingi Milion 890 na vikundi 8 vya Walemavu Milioni 157.
Maonyesho hayo yamehudhuriwa na pia na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Wabunge wa majimbo ya Ilala, Segerea na Ukonga, Mstahiki meya Ilala, Katibu tawala wa Ilala na watu mbalimbali.