Home SPORTS RAIS WA UEFA AFURAHISHWA NA FURSA ZA UWEKEZAJI ZILIZOPO TANZANIA

RAIS WA UEFA AFURAHISHWA NA FURSA ZA UWEKEZAJI ZILIZOPO TANZANIA

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya Aleksander Ceferin (aliyevaa tisheti nyekundu) akiangalia Madini aina ya Tanzanite yanayozalishwa Tanzania pekee wakati wa ziara yake ya kutembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya Dubai EXPO 2020 Dubai yanayoendelea Katika Jiji la Dubai Nchi za Falme za Kiarabu.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya Aleksander Ceferin (aliyevaa tisheti nyekundu) akimsikiliza Afisa Uhamasishaji Uwekezaji Mwandamizi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Latiffa Kigoda (kulia) kuhusu fursa za Uwekezaji zilizopo Tanzania. (wa pili kulia) ni Mkurugenzi wa Banda la Tanzania EXPO 2020 Dubai Bi. Getrude Ng’weshemi.

Mkurugenzi wa Banda la Tanzania Katika Maonesho ya Dubai EXPO 2020 Getrude Ng’weshemi (wa pili kutoka kulia) akimueleza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Ulaya (UEFA) Aleksander Ceferin (aliyevaa tisheti nyekundu) kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Na: Kassim Nyaki-Dubai, UAE.

Rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) Aleksander  Čeferin ametembelea banda la Tanzania katika maonesho ya Kimataifa ya Dubai EXPO 2020 yanayoendelea  katika Nchi za Falme za Kiarabu ambapo ameonesha kufurahishwa na fursa za uwekezaji zilizoko nchini Tanzania.

Čeferin ametoa kauli hiyo baada ya kupata maelezo kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania katika sekta za kilimo, utafiti, Madawa na Vifaa tiba, Maliasili na Utalii, teknolojia, uzalishaji wa Sukari  na usindikaji wa mazao katika sekta mbalimbali ambazo ni  kichocheo cha uchumi wa Tanzania.

“Nimewahi kuja Tanzania na Kutembelea maeneo ya vivutio kama Hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Mlima Kilimanjaro, leo nimejua zaidi kuwa Tanzania pia ina mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali, hii ni baraka na neema ambayo wageni wanaokuja kwenye maonyesho haya wanapaswa kutembelea banda hili kupata maelezo kuhusu vivutio vya utalii, uwekezaji na kujua uwepo wa madini mbalimbali ambayo mengine yanapatikana Tanzania pekee” amefafanua  Čeferin.

Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika maonesho hayo Bi. Getrude Ng’weshemi amemueleza Rais wa UEFA kuwa katika jitihada za kuboresha mazingira ya uwekezaji, Tanzania inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutokea bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuunganisha na nchi jirani na uboreshaji wa miundombinu katika Sekta ya Utalii.

“Tanzania inazungukwa na nchi zaidi ya 8 zikiwemo Uganda, Rwanda, Sudani ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Zambia na Malawi, na sehemu kubwa nchi hizi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam na ndio maana serikali inatumia jitihada kubwa kuboresha Bandari hiyo ya  pamoja na miundombinu ya Reli ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa bidhaa na mizigo” aliongeza Bi. Getrude

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bi. Latiffa Kigoda amemueleza Rais wa UEFA na ujumbe wake kuwa Nchi ya Tanzania inakaribisha wawekezaji katika sekta za kilimo na uongezaji thamani mazao, uzalishaji wa mafuta ya kula, uzalishaji wa sukari, nguo, uzalishaji wa madawa na vifaa tiba, mifugo na uongezaji thamani katika uzalishaji wa maziwa, usindikaji wa nyama na utengenezaji wa bidhaa za ngozi, uvuvi na usindikajj wa samaki, uzalishaji wa mbolea, na uanzishaji wa maeneo ya ukanda maalum ya uwekezaji ‘’industrial parks”

Bi Latiffa ameongeza kuwa Ili kumrahisishia mazingira ya uwekezaji Tanzania, Serikali imeanzisha Mfumo wa huduma za pamoja (One Stop Facilitation Centre), ambapo Maafisa Waandamizi wa Taasisi mbalimbali za Serikali  wanasaidia mwekezaji kupata vibali, leseni na idhini katika sehemu moja (one stop Centre). 

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni TIC, Wizara ya Ardhi, TANESCO, BRELA, TRA, NEMC, OSHA, TMDA, NIDA, Uhamiaji, Wizara ya Kazi na TBS.

Miongoni mwa taasisi za Tanzania zinazoshiriki maonyesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Abu Dhabi katika Nchi za falme za Kiarabu.

Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza tarehe 01 oktoba, 2021 yanaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Machi, 2022.

Previous articleMIGOGORO YOTE YA ARDHI WILAYANI IKUNGI MKOANI SINGIDA KUMALIZWA
Next articleKUTOKA MEZA YA MAGAZETI ASUBUHI YA LEO ALHAMISI DISEMBA 30-2021
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here