Katika Kuelekea Miaka 60 ya Uhuru- Mhe. Rais Samia azindua Kiwanda cha kutengeneza Nyaya za Mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing Tanzania Ltd- Pia azungumza na wananchi wa Mbagala (DSM) na Vikindu mkoani Pwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizindua Kiwanda cha kutengeneza Nyaya za Mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing Tanzania Limited kilichopo Mkuranga mkoani Pwani leo tarehe 03 Desemba, 2021. Wengine katika picha kutoka kulia wa kwanza ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Geoffrey Mwambe pamoja na Mtendaji Mkuu wa Kiwanda hicho Ramadhani Hassani Mlanzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kama ishara ya kuzindua Kiwanda cha kutengeneza Nyaya za Mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing Tanzania Limited kilichopo Mkuranga mkoani Pwani leo tarehe 03 Desemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua kazi mbalimbali katika Kiwanda cha kutengeneza Nyaya za Mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing Tanzania Limited kilichopo Mkuranga mkoani Pwani leo tarehe 03 Desemba, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha kutengeneza Nyaya za Mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing Tanzania Limited wakati akipita kukagua hatua mbalimbali za utengenezaji wa nyaya hizo za Mawasiliano Fiber katika kiwanda hicho kilichopo Mkuranga mkoani Pwani leo tarehe 03 Desemba, 2021.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 03 Desemba, 2021 amezindua Kiwanda cha kutengeneza Nyaya za Mawasiliano cha Raddy Fiber Manufacturing Ltd kilichopo katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho, Mhe. Rais Samia amesema hafla hiyo ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara ambapo ameanza kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika baadhi ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Rais Samia amesema uzinduzi wa kiwanda hicho unathibitisha uwezo na fursa nyingi ambazo nchi imejaliwa kuwa nazo na ziweze kutumika ili kukuza uchumi wa nchi, kuleta ajira kwa wananchi hususan vijana na kuzalisha bidhaa ambazo sio lazima kuagizwa kutoka nje.
Aidha, Mhe. Rais Samia amemshukuru na kumpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho Bw. Ramadhani Hassani Mlanzi ambaye ni mzawa kwa kuona kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza na kumhakikishia kuwa Serikali itampa ushirikiano wa kutosha.
Mhe. Rais Samia amewakaribisha wawekezaji wengine kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza Tanzania na kuwahakikishia usalama wa mitaji yao pamoja na uhakika wa kutengeneza faida.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi nchini katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi hivyo inaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
Mhe. Rais Samia ameagiza taasisi zote za Serikali zinazotoa huduma katika sekta ya Uwekezaji kuondoa urasimu ambao umesababisha kupoteza baadhi ya wawekezaji waliokuwa wanataka kuwekeza nchini kwa kuwa wawekezaji wana mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi yetu.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amesema Serikali itaimarisha jitihada za mageuzi ya kisera na kisheria ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini ujulikanao kama The Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Enviroment.
Mhe. Rais Samia amesema Serikali ina lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafikiwa na huduma za mawasiliano ili kuwawezesha kutumia huduma zitonakazo na TEHAMA katika kukuza uchumi nchini.
Aidha, Mhe. Rais Samia amemtaka Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Raddy Fiber Manufacturing Ltd kuhakikisha kuwa anakamilisha azma yake ya kujenga kiwanda cha kuzalisha simu janja (smart phone) hapa nchini ambacho pia kitachangia utoaji ajira kwa vijana.
Kiwanda cha Raddy Fiber Manufacturing Ltd kina uwezo wa kuzalisha kiasi cha kilomita 24,000 za optic fiber kwa mwaka na kinatarajiwa kutoa ajira zipatazo 670 kitakapokamilika katika awamu zote na hivyo kukifanya kuwa kiwanda cha tatu kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza kwa Afrika Mashariki na Kati.
Awali akiwa njiani kuelekea Mkuranga, Mhe. Rais Samia alipata fursa ya kuwasalimia wananchi wa Mbagala Zakhem na Vikindu mkoani Pwani ambapo amewahakikishia wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga kuwa kwa sasa Serikali inajenga mazingira bora zaidi ambayo yatawawezesha kufanya biashara kwa uhuru na katika msimu wote wa mwaka.