Home BUSINESS PROF. KITILA MKUMBO: WAJASIRIAMALI WANAWAKE TEGEMEO KUBWA KATIKA FAMILIA

PROF. KITILA MKUMBO: WAJASIRIAMALI WANAWAKE TEGEMEO KUBWA KATIKA FAMILIA

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof Kitila mkumbo akisikiliza maelezo ya matumizi Mashine aina ya Chopa kutoka katika Banda la Wajasiriamali kutoka Kenya, Mashine hii inauwezo wa kusaga magunzi ya mahindi na kuwa katika mfumo wa unga kwaajili ya chakula cha mifugo, pia ina uwezo wa kusaga nafaka mbalimbali.

Waziri wa Viwanda na Biashara Prof Kitila mkumbo akipokea picha iliyochorwa mfano wa sura yake kutoka kwa Mchoraji na Msanii Melisa N. Kazina kwenye Banda la wenyeji Tanzania leo tarehe 05 Disemba,2021.


Na: Judith Ferdinand,Mwanza

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa.Kitila ni Mkumbo amesema asilimia 90 ya mapato ya biashara zinazofanywa na wajasiriamali wanawake yanarudi kusaidia familia na kutatua changamoto za chakula, matibabu na elimu.

Amesema kuwa mapato hayo ni  fursa ya kuvunja umasikini na kuwapa wanawake nafasi ya kufanya biashara huku tafiti zikionesha mapato ya wanaume ni chini ya asilimia 50 na kuhoji zaidi ya asilimia 50 yanakwenda wapi.

Profesa .Mkumbo ametoa kauli hiyo  Tarehe 05 Desemba 2021 wakati akifungua maonesho ya 21 ya wajasiriamali  wadogo na wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali yanayofanyika  Rock City Mall mkoani Mwanza.

Prof Kitila ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maonesho hayo amemwakilisha  Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa asilimia  6O ya washiriki katika maonesho hayo ni wanawake hivyo mapato yao yataenda kusaidia katika familia zao katika masuala ya chakula,matibabu na elimu ya watoto hivyo mapato hayo ni fursa ya kuvunja mnyororo wa umasikini.

“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwani nchi zote duniani ujasiriamali unachukua nafasi  kubwa ,naomba nisahihishe hapa hakuna mfanyabiashara mdogo kuna biashara ndogo na biashara ya kati” amesema Prof. Mkumbo.

Kuhusu wajasiriamali Prof.Mkumbo amesema  vijana ndio matajiri  wakubwa  watarajiwa  ambao kwa upande  wa Tanzania wamefanya utafiti wa viwanda na biashara uzalishaji bidhaa asilimia 98 unatokana na viwanda vidogo sana na vidogo. 

Akizungumzia suala la kuwawezesha wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,Prof.Mkumbo amesema serikali zote  za nchi hizo zimekubaliana kuwa na sera moja za kuendeleza wajasiriamali wadogo na wa kati.

Pia wataendelea kufanya kazi ya kuondoa vikwazo vinavyo kwamisha wafanyabiashara katika Jumuiya hiyo.

“Tuwaunge mkono viongozi wetu,ambao ambao wamepanga  kuona  mazingira ya kufanyia biashara  yana kwenda kuboreshwa , wajasiriamali kuweni wabunifu ambao ubunifu huo pia tumeuona kwa wajasiriamali wetu katika maonesho haya,” amesema Prof.Mkumbo.

Aidha amesema,lengo la serikali ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ili wazalishe bidhaa za kutosheleza mahitaji ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tumeona namba kubwa ya wanawake na vijana wamejitolea kuzalisha bidhaa za ubunifu, serikali itahakikisha inawekeza nguvu katika uwezeshaji wao ili kuhakikisha viwanda vyetu vinapata malighafi ya kutosha inayozalishwa na wazalishaji wadogo na wa kati,” amesema Prof.Mkumbo.

Nae mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali wa Jumuiya ya aAfrika Mashariki Josephat Rweyemamu,amesema maonesho hayo yalianza mwaka 1999 yakiwa na washiriki 59 Sasa wameongezeka Hadi kufikia takribani wajasiriamali 1400 pia bidhaa zimeongezeka na zingine zimepata nembo za ubora.

Akitoa salamu za Mkoa wa Mwanza Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel,amesema jumla ya wajasiriamali 1,304 wamethibitisha  ushiriki kati ya hao 794 wametoka katika nchi za Kenya,Uganda,Sudan ya Kusini,Burundi,Rwanda na 510 kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

“Maonesho haya kwetu sisi kwa  wanamwanza  ni fursa ya kipekee ya kuandika historia ya Mkoa wetu wa Mwanza,yamesaidia kukua kwa pato la taifa  na wajasiriamali,pia kupitia mzunguko wa fedha utasaidia Mkoa kuongeza pato,” na kuongeza kuwa 

“Nindelee kutoa wito kwa wananchi wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kujitokeza kutembelea mabanda na kununua bidhaa kwa kufanya hivyo tunainua uchumi wetu na kuendelea kutangaza bidhaa za wajasiriamali wa Jumuiya hii,”amesema Mhandisi Gabriel.

Mhandisi Gabriel amesema kuwa Mwanza ni eneo lenye ardhi nzuri na uchumi ,kuna maeneo mbalimbali ya uwekezaji na yakibiashara hivyo wafanyabiashara wajitokeze kuwekeza.

Ameongeza kuwa hakuna rushwa wala kuzungushana katika upatikanaji wa maeneo huku akitia wito kwa wananchi kujitokeze kwa wingi katika maonesho hayo ili kukuza uchumi na kuzitangaza bidhaa mbalimbali za Afrika Mashariki.

Nae  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira Walemavu), Jenista Mhagama akiongea wakati anamakribisha mgeni rasmi amesema, tatizo la ajira ni kwa wote hivyo maonesho hayo ni ufunguo wa ajira, kukuza uchumi pia ni nyenzo ya kubadilishana ujunzi ambao unaweza  kutengeneza ajira nyingi nchini pamoja na kubadilishana elimu ya ujasiriamali na kudumisha umoja na mshikamano.

“Maonesho haya  yanaendana sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru  na kuonesha  thamani ya uwepo wetu,kutumia rasilimali tulizonazo,kutumia teknolojia na ujuzi kidogo lakini tukaboresha bidhaa,ambazo zinaweza kuingia kwenye masoko makubwa ya  kimataifa,”amesema Mhagama

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Wajasiriamali nchini Kenya David Osiany,amesema anafarijika kuona akinamama na vijana wajasiriamali kwenye maonesho ya mwaka huu ambapo nchini Kenya sekta hiyo inachangia  asilimia 83 ya ajira.

Amesema maonesho ya wajasiriamali yanatoa fursa kuonesha dunia kuwa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki si watu wa kununua bidhaa za nje ya nchi zao bali wanao ujuzi wa kutengeneza bidhaa zenye ubora.

Mwisho.


.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here