Home SPORTS MHE. GEKUL AWATAKA VIONGOZI TSA KUENEZA MCHEZO NCHI NZIMA

MHE. GEKUL AWATAKA VIONGOZI TSA KUENEZA MCHEZO NCHI NZIMA


Na: Stella Kessy, DAR ES SALAAM.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo amewataka Viongozi wa chama cha mchezo wa kuogelea Nchini (TSA) kuhakikisha mchezo wa kuogelea unasambaa nchi nzima, mikoani na wilayani ili kupata waogeleaji wenye vipaji watakaoiwakilisha vema Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akikabidhi bendera na kuiaga timu ya Tanzania inayokwenda kushiriki mashindano  ya kuogelea ya Kanda ya tatu (Zone 3)  yanayotarajiwa kuanza tarehe 09 Disemba, 2021 nchini Uganda.

Katika tukio hilo Mhe.Gekul ameambatana na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo BMT Neema Msitha pia aliwapongeza wazazi kwa kuwaruhusu watoto kushiriki katika  mchezo huu.

“Niwapongeze wazazi kwa mwamko mkubwa wa kuwarushusu watoto kujiunga kwenye mchezo huu, hii itasaidia kupata vipawa na vipaji vingi “ amefafanua Mhe. Gekul

Alisema Serikali imeshaandaa Mpango Mkakati wa miaka kumi wa kuinua na kuendeleza michezo na kuainisha michezo 6 ya kipaumbele ya kuanza nayo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msitha amemweleza  Naibu Waziri kuwa chama cha  mchezo wa kuogelea ni miongoni mwa vyama vya michezo  inayofanya kazi nzuri ya kuinua mchezo huu hapa nchini.

Awali Katibu Mkuu wa TSA Inviolata Itatilo alisema nchi zaidi ya kumi zinatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo nchini Uganda.

Wachezaji wa Tanzania wanatarajia kuondoka kesho tarehe 05 Disemba, 2021 kuelekea nchini Uganda na inapeleka waogeleaji 26, wavulana 16 na wasichana 10.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here