Na: WAMJW – Dar Es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19 hususan wanapokua kwenye mikusanyiko.
Rai hiyo ameitoa leo wakati alipotembelea kituo cha mabasi ya mwendokasi kilichopo gerezani jijini Dar es Salaam pamoja na kivuko cha meli Kigamboni.
Prof. Makubi wakati wa ziara zake hizo pia ameweza kutoa elimu kwa wasafiri kwenye maeneo hayo ili waweze kujikinga na maambukizi ya Magonjwa ya milipuko ikiwemo la UVIKO-19.
“Mliopata hii elimu endeleni kuzingatia haya na elimu inayotolewa juu ya kijikinga na mnapaswa kuwa mabalozi wazuri wa kwenda kuwaelimisha wengine”
“Wazee wetu nyumbani wenye magonjwa yasiyo yakuambukiza wapo kwenye hatari kubwa ya kupata Covid-19, sisi wenyewe tujikinge ili tuwakinge wengine ambao tumewaacha majumbani”Amesema Prof. Makubi
Hata hivyo Prof. Makubi aliwaasa wananchi hao kuendelea kunawa mikono kwa maji tiririka na kuvaa barakoa wanapokuwa kwenye maeneo hatarishi na yenye mikusanyiko ikiwemo standi, kwenye ibada, vyuoni,viwanja vya ndege na maeneo mengine yenye watu wengi.
Vile vile Prof. Makubi aliweza kukagua miundombinu ya maeneo hayo na kuwakumbusha viongozi kuhakikisha kunakuwa na maeneo ya kunawa mikono yanakuwa na maji na sabuni wakati wote.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuona jinsi gani wananchi wanaendelea kuchukua tahadhari juu ya UVIKO-19.
Dkt. Mfaume amesema ugonjwa huo bado upo duniani hivyo ni lazima tahadhari zichukuliwe ikiwemo kuachiana nafasi angalau umbali wa mita moja, kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara