Na: Mwandishi wetu, Dar.
MABINGWA wa kihistoria Yanga SC leo wameibuka na ushindi wa bao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Ruvu Shooting walitangulia kwa bao la Shaaban Msala dakika ya tisa akimalizia pasi ya Nathaniel Chilambo, kabla ya Yanga kupambana na kupindua meza.
Kiungo Feisal Salum alianza kuisawazishia Yanga dakika ya 32, kabla ya Wakongo, beki Djuma Shabani kufunga la pili dakika ya 48 kwa penalti na kiungo Mukoko Tonombe kufunga la tatu dakika ya 75 akimalizia kazi nzuri ya kiungo mzawa, Farid Mussa.
Hata hivyo kikosi cha Ruvu Shooting inachofundishwa na kocha Charles Mkwasa ilimaliza pungufu baada y mchezaji wake, Santos Mazengo kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 24.
Kikosi cha Yanga leo wanafikisha pointi 15 baada ya kushinda mechi zote tano tangu msimu uanze na kuendelea kuongoza ligi kwa pointi tano zaidi ya Polisi Tanzania wanaofuatia wakati Ruvu Shooting inabaki na pointi zake sita za mechi tano sasa.