Na: Stella Kessy.
VINARA, Yanga SC leo wametoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo katika Ligi Kuu ya Tanzania katika uliopigwa dimba la Ilulu mjini Lindi.
Katika mchezo uliokuwa na ushindani kwa timu zote ambapo mpaka kufika hatua ya mapumziko hakuna timu iliyoona lango la mpinzani wake
Katika dakika za 53 mshambuliaji, Obrey Chirwa aliipatia namungo bao,Pia katika dakika za 82 kiungo Saido Ntibanzokiza kumfunga Mrundi mwenzake, kipa Jonathan Nahimana kwa penalti.
Yanga inafikisha pointi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC baada ya timu zote kucheza mechi sita.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Geita Gold wamewachapa wenyeji, Kagera Sugar 2-1 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mabao ya Geita yamefungwa na George Mpole yote dakika ya kwanza na 35, wakati la Kagera limefungwa na Mbaraka Yussuf dakika ya 11.
Geita inafikisha pointi tano na kujiinua kidogo kutoka nafasi ya 15 hadi ya 13 kwenye Ligi ya timu 16, wakati Kagera Sugar inabaki na pointi zake nane katika nafasi ya sita baada ya wote kucheza mechi sita.
Nayo Mbeya City imeshinda 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya. Mabao ya Mbeya City yamefungwa na Juma Luizio dakika ya 45, Juma Shemvuni dakika ya 60 na Suleiman Ibrahim dakika ya 85, wakati la Mtibwa limefungwa na Salum Kihimbwa dakika ya 82 kwa penalti.
Kwa ushindi huo, Mbeya City inafikisha pointi 10 na kupanda nafasi ya tatu ikiizidi wastani wa mabao tu Polisi Tanzania baada ya wote kucheza mechi sita, wakati Mtibwa inabaki na pointi zake mbili za mechi sita sasa katika nafasi ya 14 kwenye Ligi ya timu 16.
Mtibwa inazizidi wastani wa mabao tu Geita Gold na KMC zilizo chini yake mkiani kwenye eneo la kushuka moja kwa moja.