Home BUSINESS “WATUMISHI ZINGATIENI SHERIA, TARATIBU NA MIONGOZO KUEPUSHA KUFANYA MAKOSA”DKT.FRANCIS

“WATUMISHI ZINGATIENI SHERIA, TARATIBU NA MIONGOZO KUEPUSHA KUFANYA MAKOSA”DKT.FRANCIS

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael amewataka watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na watumishi wote wa umma kwa ujumla, kufuata kanuni, taratibu, sheria pamoja na miongozo ya utumishi wa umma katika utendaji kazi wao wa kila siku ili kuepuka kutokufanya makosa ya kiutumishi.

Dkt. Michael ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Novemba, 2021 alipofanya ziara katika taasisi ya BRELA ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa Wizara yao ya menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, kutembelea ofisi na taasisi za Serikali ili kujua changamoto na matatizo yanayowakabili watumishi wa umma katika sehemu zao za kazi.

Dkt. Michael amesema watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu ambazo zimewekwa kuepuka makosa ya kiutumishi

Dkt. Michael ameeleza kuwa Maafisa Utumishi wanawajibu wa kuwa na nyaraka zote za kiutumishi na kuhakikisha kuwa watumishi wote wanazifahamu nyaraka hizo kwa kuwa siyo nyaraka za siri, hii itasaidia watumishi kujua haki, stahiki pamoja na wajibu wao na kuondoa uwezekano wa watumishi kufanya makosa ya kiutumishi kwa kutokutambua sheria na miongozo inayowasimamia, lakini pia, aliongeza kusema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko ya watumishi mahala pa kazi.

“Mtumishi anapokuwa na malalamiko ya kiutumishi morali ya kufanya kazi hupotea na hata malengo yaliyotakiwa kufikia na taasisi husika hayafikiwi kikamilifu, ndio maana sisi viongozi kutoka utumishi tunaona ni bora tuwe tunawazungukia watumishi ili kuweza kuwafikia kwa ukaribu na kusikiliza shida zao na kuyatatua mapungufu madogo madogo ambayo tunaona yanaweza kutekelezwa papo kwa papo tunayafanyia maamuzi,” ameeleza Dkt. Francis

Pia, watumishi wa BRELA wameelekezwa kuheshimu mamlaka kwa kufuata maadili na viongozi wanaowasimamia watumishi wa umma kutotakiwa kunyanyasa watumishi walioko chini yao kwa namna yoyote ile. Akaongeza kusema kuwa viongozi watambue kila mtumishi anatumia muda mwingi eneo la kazi na siyo nyumbani, hivyo kila kiongozi anawajibu wa kujenga mazingira mazuri sehemu zao za kazi ili watumishi waweze kufurahia kazi.

Dkt. Michael amesema kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iko wazi kwa watumishi wote na itaendelea kutembelea taasisi za umma ili kusikia matatizo yao kwa lengo la kujenga na kuinua morali ya kazi kwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa ameeleza kufurahishwa kwa ujio wa Naibu Katibu Mkuu kwani imekuwa ni fursa nzuri ya kukutana na watumishi na watumishi wamepata nafasi ya kueleza changamoto zao kwa uwazi na kupatiwa ufumbuzi papo kwa papo.

Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano- BRELA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here