Home BUSINESS WAJASIRIAMALI WADOGO NA WA KATI WAHAMASISHWA KUSHIRIKI MAONESHO YA 21 YA NGUVU...

WAJASIRIAMALI WADOGO NA WA KATI WAHAMASISHWA KUSHIRIKI MAONESHO YA 21 YA NGUVU KAZI/JUA KALI JIJINI

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Robert Gabriel akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki (Nguvu Kazi/ Jua Kali) hii leo Novemba 25, 2021 Jijini Mwanza.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Robert Gabriel (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Msaidizi Uratibu na Uwezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Eliakim (kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Tanzania Bw. Joseph Rweyemamu (katikati) mara baada ya mkutano huo uliofanyika hii leo Novemba 25, 2021 Jijini Mwanza.

PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

Na: Mwandishi Wetu – MWANZA

Wajasiriamali Wadogo na wa Kati nchini wamehasishwa kushiriki kwa wingi kwenye Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika Desemba 2 hadi 12 mwaka huu, katika viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa huo wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel wakati wa mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi yake hii leo Novemba 25, 2021.

Alieleza kuwa maonesho hayo ya 21 ambayo hujulikana kama maonesho ya Jua Kali au Nguvu Kazi yatafanyika nchini Tanzania yanalenga hasa wajasiriamali Wadogo na wa Kati waliopo katika sekta isiyo rasmi ili kuwawezesha kurasimisha shughuli zao kwa kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa pamoja na kuongeza fursa za ajira za staha kwa vijana.

“Serikali inayachukulia maonesho haya kama fursa ya kuwawezesha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati pamoja na vijana wabunifu kutangaza kazi zao na kutafuta masoko kwa wenzetu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema

Aliongeza kuwa Maonesho hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa pamoja zimejipanga kutekeleza azma ya Serikali katika kukuza fursa za ajira hususan kwa wajasiriamali, vijana wabunifu wa makundi yote wakiwemo wenye Ulemavu.

“Maonesho haya hufanyika sambamba na makongamano ya kuwajengea uwezo wajasiriamali na wabunifu kuhusu masoko, ubora wa bidhaa, urasimishaji biashara na kuongeza thamani ya bidhaa, hivyo ni vyema wajasiriamali na vijana wabunifu nchini wakatumia fursa hii kujiletea maendeleo,” alieleza

Sambamba na hayo alieleza kuwa Fomu za maombi pamoja na maelekezo kwa wajasariamali na wabunifu wanaokusudia kushiriki maonesho hayo zinapatikana katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kupitia Afisa Biashara, Halmashauri zote nchini na Ofisi za Mameneja wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ambapo muda wa kurejesha fomu hizo ni Novemba 28, 2021.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Robert Gabriel alitimia fursa hiyo kusisitiza Kamati ya Uratibu kuhakikisha inaibua na kuteua wajasiriamali na vijana wabunifu kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa. Pia amehamasisha wajasairiamali na vijana wabunifu kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo. Pamoja na hayo alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi kutembelea maonesho hayo na kujionea bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa maonesho hayo hayana kiingilio.

“Tumejipanga katika kuhakikisha masuala ya afya yanazingatiwa wakati wote wa maonesho hususan kuchukua tahadhari dhidi ya changamoto ya UVIKO – 19,” alisema

Kauli mbiu ya Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ni: Kuhamasisha ubora na uvumbuzi ili kuongeza Ushindani wa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki na hatimaye kuwainua kiuchumi hasa kutokana na janga la UVIKO 19

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here