Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Posta Burundi Bi. Lea Ngabire akisaini Kitabu cha Wageni wakati alipotembelea Makumbusho ya Mawasiliano iliyopo Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Katika ziara hiyo ya mafunzo Ingabire aliambatana na Maafisa Waandamizi wa Posta Burundi. Picha na: TCRA
Na: Mwandishi wetu
Shirika la Posta la nchini Burundi limeweka bayana dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya Posta nchini humo ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi zaidi katika usimamizi wa masuala ya Posta.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya posta wa Burundi Bi. Lea Ngabire wakati alipozuru Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania akiambatana na ujumbe wa Maafisa waandamizi wa Posta Burundi katika ziara ya mafunzo.
“Tumefika hapa TCRA na kujionea shughuli mbalimbali za mawasiliano na lengo letu ni kuona namna nchi zetu mbili zinavyoweza kushirikiana katika kukuza na kuendeleza sekta ya posta” alibainisha Ngabire.
Ujumbe wa Maafisa hao umejumuisha Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Posta Burundi Nyayishimiye Olivier na Mkuu wa masuala ya Barua Misirakuba Deo.
Akipokea ujumbe huo mnamo Jumatano Tarehe 17 Novemba 2021 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari aliwakaribisha na kuwaeleza kuwa TCRA kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano nchini Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa mawasiliano hasa kikanda na imekuwa mshirika muhimu wa mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inasimamiwa kwa uthabiti na kwa upande wa posta TCRA imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa na kama mnavyofahamu pia Makao Makuu ya Posta Afrika yapo hapa nchini” alibainisha na kuongeza Jabiri.