Home BUSINESS TANZANIA HUTUMIA NUSU TRIONI KUAGIZA MAFUTA YA KULA.

TANZANIA HUTUMIA NUSU TRIONI KUAGIZA MAFUTA YA KULA.



Na: Lucas Raphael,Singida

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema kwamba Tanzania hutumia Nusu Trioni kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula kutoka nchi za nje Jambo ambalo kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kulifanyia kazi kwa kasi kwa kusimamia kilimo cha Alizeti na mazao mengine ya mafuta.

Kauli hiyo alitoa jana Mkoani Singida wakati akizindua zoezi la ugawaji wa Mbegu za Alizeti kupitia mradi wa kupambana na madhara ya janga la UVICO 19 chini ya ufadhili wa IFAD.

Prof. Adolf Mkenda alisema kwamba serikali imejipanga kuhakikisha wakulima wanapata Mbegu bora za Alizeti ili kuweza kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi wakati ndani ya nchi uwezo wa uzalishaji upo.

“Sisi Kama wizara tutahakikisha tunapunguza kama sio kumaliza tatizo hili la uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kwa sababu tuna maeneo makubwa na hali ya hewa ambayo ni rafiki kwa zao hili la Alizeti. Hivyo tunaendelea kuweka nguvu”. Amekaririwa Prof Mkenda.

Waziri Mkenda alisema mradi huo wa IFAD utasaidia wakulima wa alizeti kupata mbegu hasa katika mikoa ya kimkakati ambayo imepangiwa malengo na Serikali katika kuzalisha zao hilo.

Mkenda alipongeza Jackline Machangu Msimamizi Mkuu wa mradi wa IFAD Nchini kwa kuwa mzalendo pamoja na kupambana kuhakikisha mradi huo unafanikiwa hapa Nchini.

Kwa upande wake Jackline Machangu ambaye ni Msimamizi Mkuu wa mradi wa IFAD Nchini amesema kuwa IFAD itahakikisha ina simamia kwa ukamilifu mradi huo wenye lengo la kuwafikia jumla ya wakulima zaidi ya 6000 ambao kati yao wakulima zaidi ya 4000 ni wakulima wa zao la alizeti, ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika mradi huo.

Aliipongeza wizara ya kilimo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha hasa katika suala hili la Mbegu za Alizeti ambazo zinaendelea kusambazwa kwa wakulima kupitia Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA).

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA ) Dkt Sophia Kashenge alisema kuwa ASA Inafanya kazi kwa karibu na mradi huo wa IFAD ambapo kupitia mradi huo ASA itasaidi usambazaji wa kilo 13,000 za mbegu bora za hybrid aina ya SUPERSUN katika baadhi ya maeneo ya kimkakati katika mkoa wa singida, Dodoma na Simiyu.

Alisema zoezi la kusambaza mbegu za wakala kwa ujumla linaendelea kwa kasi hasa mbegu za alizeti na mazao mengine ili kuwahi msimu wa kilimo.

Alisema moja ya changamoto wanayokutana nayo Wakala ni changamoto ya usafari ambapo kwa sasa mazungumzo yameanza ili kupata magari ya jeshi la wananchi yatakayoweza kusambaza mbegu hizo kwa haraka.

Dkt Sophia Kashenge aliwataka wakulima kutumia Mbegu bora hasa mbegu za Serikali ambazo zimegunduliwa na kufanyiwa utafiti na watafiti wa TARI ambazo zinasambazwa na Wakala wa mbegu za kilimo (ASA). Mbegu hizo zinalenga wakulima wadogo na wa kati hivyo zinazouzwa kwa bei nafuu ya serikali.

Hata hivyo amewaasa wakulima kuhakikisha wanatumia kanuni bora za Kilimo ili mbegu hizo ziweze kuonyesha tija iliyokusudiwa.

Dkt Binilith Mahenge Mkuu wa Mkoa wa Singida alisema kama mkoa umejipanda kuhakikisha zao la Alizeti linalimwa kulingana na malengo waliyojiwekea kama mkoa wa singida.

Alisema tayari mpaka Sasa wameorodhesha wakulima wote wa Alizeti huku Mbegu zikiendelea kusambazwa katika Halmashauri za mkoa huo ili wananchi waweze kupata kwa bei nafuu na kwa wakati utakao kuwa rafiki kuingia shambani.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa amemuomba waziri kuongeza Mbegu katika mkoa wake kutokana na wahitaji kuwa wengi tofauti na idadi iliyotengwa kwa mkoa huo wa singida.

DKT Mahenge ameipongeza wizara ya kilimo kwa kuonesha juhudi kubwa ya kupambana na tatizo la upungufu wa mafuta hasa kwa kuhimiza na kuweka mikakati ya kilimo cha Alizeti na mazao mengine ya mafuta kama vile michikichi.

MWISHO.

 

Previous articleMAKAMBA AZISHUKURU NORWAY SWEDEN NA SAUD ARABIA
Next articleMHE. MARY MASANJA AWATAKA ASKARI UHIFADHI KUFANYA KAZI KWA UADILIFU
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here