Wafanyabiashara wamehimizwa kutumia fursa ya kuuza bidhaa zao kupitia Duka la Mtandaoni (E–SHOP) ili bidhaa hizo ziweze kutangazika na kufanya mauzo ndani na nje ya nchi.
Nora Mishiri ni Afisa Rajam mwandamizi wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) anasema kuwa Duka hilo lilizinduliwa rasmi mwezi Julai mwaka huu ambalo lilikuwa na lengo la kutoa fursa kwa wafanyabiara kutangaza bidhaa zao ili ziweze kuwafikia wateja na kutanua wigo wa Biashara zao ndani na nje ya nchi.
Mishiri ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mradi wa kuwawezesha wabunifu wa Mitindo na Mavazi (Fashion for Change Program) unaosimamiwa na Chama Cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC) ambapo amesema kuwa mpaka sasa tayari kuna bidhaa zaidi ya 200 kwenye Duka hilo ambazo zinafanya vizuri.
“Mpaka sasa Duka hili lina bidhaa zaidi ya 200 ambazo zimeendelea kufanya vizuri na tunaamini taratibu tunaenda vizuri kwani kuna muamko kwa wafanyabisha kujiunga kwenye E-SHOP” Amesema Norah.
Amesema kuwa wao kama TANTRADE wameendelea kutoa elimu kwa wafanayabishara juu ya umuhimu wa kulitumia jukwaa hilo lenye uwezo wa kumfikia mteja popote alipo Duniani na kwamba uhamasishaji unaendelea kwa kuweka mikakati mbalimbali ya namna wafanyabiashara kuingiza Bidhaa zao kwenye Duka hilo.
“Tunaendelea kuhamasisha na tayari ipo mikakati ambayo imewekwa kwaajili ya kuwaaeleza wafanyabiashara namna ya kutumia hili jukwaa, hivyo wafanyabishara waitumie fursa hii itakayowasaidia kutangaza Bidhaa zao na kunufaika” Ameongeza Nora.
Duka hilo la Mtandaoni (E-SHOP) lilizinduliwa rasmi mwezi julai mwaka huu wakati wa Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) na Waziri wa Viwanda na Biashara Pro. Kitila Mkumbo na Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dr. Faustine Ndugulile (Mb) ambapo Duka hilo lipo chini ya uangalizi wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE), na Shirika la Posta Tanzania (TPC).