Home BUSINESS TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA ZA KUDHIBITI KUONGEZEKA KWA MIKOPO CHECHEFU ...

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HATUA ZA KUDHIBITI KUONGEZEKA KWA MIKOPO CHECHEFU KATIKA SEKTA YA BENKI

 

Benki Kuu ya Tanzania imefanya utafiti katika sekta ya benki na kubaini sababu kubwa  za kuongezeka kwa mikopo chechefu ni kutokana na wafanyakazi wa baadhi ya benki na  taasisi za fedha kuhusika moja kwa moja kwa kutoa mikopo bila kuzingatia taratibu, kukosa uadilifu, na kushirikiana na wakopaji katika kutoa mikopo kiuhalifu, ikiwemo  vitendo vya rushwa. 

Ikumbukwe kuwa kuongezeka kwa mikopo chechefu katika sekta ya  benki ni moja ya sababu kubwa ya benki na taasisi za fedha kutoza viwango vikubwa  vya riba za mikopo na hivyo kuhatarisha uimara wa sekta ya benki na kuathiri uchumi wa  nchi. 

Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania inautaarifu umma kwamba imelazimika kuchukua hatua  zifuatazo katika kudhibiti vitendo vinavyopelekea kuongezeka kwa mikopo chechefu  katika sekta ya benki: 

  1. Kuendelea kufanya ukaguzi wa benki na taasisi za fedha ili kubaini sababu za  kuongezeka kwa mikopo chechefu na wafanyakazi ambao wanahusika moja kwa  moja na kadhia hiyo. 
  2. Iwapo itathibitika kuwa kuna mfanyakazi wa benki anahusika katika kutoa mikopo bila kuzingatia taratibu, kukosa uadilifu, na kushirikiana na  wakopaji katika kutoa mikopo kiuhalifu, na vitendo vya rushwa, benki au taasisi ya  fedha husika itatakiwa kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mfanyakazi huyo  na Benki Kuu ya Tanzania itamfungia mfanyakazi huyo kuajiriwa na benki au taasisi  yoyote ya fedha inayoendesha shughuli zake nchini Tanzania; 
  3. Kuzitaka benki na taasisi za fedha ambazo wafanyakazi wake wana mikopo  chechefu katika benki au taasisi za fedha nyingine kuwasilisha taarifa zao katika  taasisi za kuchakata taarifa za mikopo (credit reference bureau). Pia, Benki Kuu ya  Tanzania itawazuia wafanyakazi husika kupata ajira katika benki au taasisi yoyote  ya fedha inayosimamiwa na Benki Kuu, endapo itabainika kwamba kushindwa kwao  kurejesha mikopo kumetokana na uzembe, uhalifu au kukosa uadilifu; 
  4. Kuzitaka benki na taasisi za fedha kutokutoa mikopo kwa wakopaji wasio waaminifu  au ambao wanakopa kwa kutumia njia za udanganyifu na kuacha kulipa. Taarifa za  wakopaji wa aina hii zitatunzwa katika rejesta maalum na benki na taasisi za fedha  

zitapewa orodha yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa hawapati mikopo katika sekta  ya benki. Kwa sasa, wakopaji wa aina hii wanapewa muda wa miezi mitatu, kuanzia  tarehe ya taarifa hii, kufanya mipango ya kurejesha mikopo yao kabla majina yao  hayajaingizwa katika rejesta maalum na benki na taasisi za fedha kupewa orodha  hiyo; na 

  1. Kuzitaka benki na taasisi za fedha kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wa umma  ambao wana mikopo chechefu ili hatua stahiki zichukuliwe. Aidha, taarifa za  wakopaji kama hao nazo zitaingizwa katika rejesta maalum, na benki na taasisi za  fedha zitapewa orodha yao ili kuhakikisha kwamba hawapati tena mikopo hadi  hatua stahiki zimechukuliwa dhidi yao na wameanza kurejesha mikopo yao.  

Benki Kuu ya Tanzania inatoa wito kwa wananchi wote ambao wana mikopo kutimiza  wajibu wao wa kisheria wa kurejesha mikopo wanayokopa katika benki na taasisi za  fedha. Aidha, wananchi wanahamasishwa kutoa taarifa katika benki na taasisi za fedha au Benki Kuu kuhusu vitendo vya uhalifu au rushwa wanavyokutana navyo wakati  wanapohitaji huduma kutoka katika benki au taasisi ya fedha. Benki Kuu itaendelea  kuwasiliana na benki na taasisi za fedha kuhakikisha taratibu za utoaji mikopo  zinazingatiwa kikamilifu kwa lengo la kidhibiti kuongezeka kwa mikopo chechefu.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here