Home LOCAL SERIKALI, UNESCO YAKUTANISHA WADAU KUJADILI MKAKAKATI WA KUTOKOMEZA UKATILI KWENYE VYUMBA VYA...

SERIKALI, UNESCO YAKUTANISHA WADAU KUJADILI MKAKAKATI WA KUTOKOMEZA UKATILI KWENYE VYUMBA VYA HABARI

Washiriki wa kikao kikao kazi cha kuandaa mkakati wa kitaifa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ndani ya vyumba vya habari wakijadili jambo wakati wa ufunguzi wa kikao kinachoendelea jijini Arusha.

Mkurugenzi Msaidizi-Usajili wa Magazeti Idara ya Habari MAELEZO Bw. Patrick Kipangula akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi ha kuandaa mkakati wa kitaifa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ndani ya vyumba vya habari kinachoendelea jijini Arusha.

Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bw. Joel Mangi, akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi ha kuandaa mkakati wa kitaifa wa kupambana na ukatili dhidi ya wanawake ndani ya vyumba vya habari kinachoendelea jijini Arusha.

Na: Beatrice  Sanga-MAELEZO

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) imeandaa kikao cha wadau mbalimbali chenye lengo la kujadili namna ya kuhusisha vyombo vya Habari katika kuimarisha mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya waandishi wa Habari wanawake ndani ya vyumba vya Habari.


Kikao hicho kinachoendelea kufanyika Jijini Arusha kimehusisha wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Wizara ya Afya, Maendeleo  ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, TAMISEMI, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), waandishi wa Habari na wadau wengine wa kupigania haki za waandishi wa Habari wanawake.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Mkurugenzi Msaidizi -Usajili wa magazeti- Idara ya Habari Bw.Patrick Kipangula  amesema anatarajia kikao hicho kitoke na mpango utakaowezesha kuwa na mkakati wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake wanaofanya kazi ndani ya vyombo vya Habari ikiwa ni Pamoja na kuwajengea uwezo waandishi wanawake kuweza kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji.


“Vyombo vya Habari  vina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu ukatili dhidi ya wanawake lakini pia waandishi wa Habari wanaofanya kazi ndani ya vyombo vya Habari wanatakiwa kuibua ukatili unaofanyika dhidi yao ili kuweza kubaini ukubwa wa tatizo na hatimae hatua Zaidi kuchukuliwa” Amesema Bw. Kipangula.


Naye Afisa Maendeleo ya jamii kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na Watoto Bw.Erasto Chimolo ameeleza kuwa Wizara toka mwaka 2018 mpaka sasa imekuwa ikiratibu Utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) na mpango huu umekuwa jumuishi na shirikishi katika kutambulishwa kwake na utekelezaji wake kwa ujumla ambapo mpango huu unaendelea kutekelezwa kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya Kiserikali, vyombo vya habari pamoja na watu binafsi.


Aidha  ameongeza kuwa vikao vya maandalizi vilivyopita ambavyo kwa pamoja vilibaini mapungufu kwenye MTAKUWWA ambapo kikao hiki kinaenda kuangalia namna nzuri ya kuweza kuja na mapendekezo ya uzingatiwaji wa maeneo ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi vizuri.


“Tumekusanyika hapa kwa pamoja ili tuweze kutoa maoni ambayo yatatusaidia kuingiza vyombo vya habari katika mpango wetu ili tunapokuwa tunaelekea kufanya tathmini ya MTAKUWWA namba mbili basi tuwe tumehakikisha kwamba suala la uanzishaji wa Afua za kudhibiti, kuratibu na kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto unazingatiwa kwa kiasi kikubwa sana”. Amesema Bw.Chimolo

 

Chimbuko la mkutano huo ni maazimio ya mkutano wa siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambao kitaifa ulifanyika Jijini Arusha Mei 3 mwaka huu wa 2021.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here