Home LOCAL RC TABORA AISHAURI TAASISI YA SAMUEL NA MARGRET SITTA KUONGEZA MASUALA YA...

RC TABORA AISHAURI TAASISI YA SAMUEL NA MARGRET SITTA KUONGEZA MASUALA YA ELIMU KATIKA MIPANGO YAO

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika bango la Taasisi ya Samuel na Margret Sitta  mara baada ya kuizindua jan.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani  akiwahutubia wananchi jana mjini Urambo kabla hajazindua Taasisi ya Samuel na Margret Sitta.

Baadhi ya Madaktari Bingwa wakiwa katika mkutano wa uzinduzi wa Taasisi ya Samuel na Margret Sitta, (Picha na Lucas Raphael)

Na: Lucas Raphael,Tabora 

MKUU wa Mkoa wa  Tabora Balozi Dkt Batilda Buriani ameishauri Taasisi ya Samuel na Margret Sitta kuongeza mipango ya kufadhili vijana katika masuala ya elimu ili kuokoa vipaji ambavyo vingeweza kupotea kwa sababu ya kuwa na kipato kidogo. 

Alitoa kauli hiyo jana wilayani Urambo wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Samuel na Margret Sitta ambayo imeanzishwa na familia ya Marehemu Samuel Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka mitano tangu kifo chake.

Alisema hatua hiyo itawasaidia kuwaendeleza vijana wengi ambao wana ufaulu wa juu lakini wanashindwa kuendelea na masomo zaidi kutokana na familia zao kushindwa kumudu gharama mbalimbali ikiwemo za nauli na ada.

“Mmefanya jambo zuri la kuanzisha Taasisi ambayo inasaidia kuwaleta Madaktari bingwa ambao watatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na kutoa matibabu kwa wakazi wa Urambo kwa siku tano…nawaomba mpanue huduma za Taasisi yenu mwende zaidi kwa kuanza kutoa Sponsorship kwa vijana ambao wamefanya vizuri na wanashindwa kuendelea na masomo” alisisitiza.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora ameishukuru Taasisi ya Samuel na Margret Sitta kwa kuwezesha kuleta wilayani Urambo Madaktari Bingwa wa Magonjwa mbalimbali 31.

Alisema kitendo hicho  kuwaleta Madaktari Bingwa kitasaidia wakazi kuwapatia huduma kama vile za uchunguzi wa magonjwa ya ndani ya uzazi, magonjwa ya wananwake, saratani, magonjwa ya macho, matatizo ya mifupa, matatizo ya masikio , pua na magonjwa ya watoto.

Mbunge wa Jimbo la Urambo Margret Sitta alisema familia yao imeamua kumuenzi Marehemu Samuel Sitta kwa kuanzisha Taasisi na kuwaleta Madaktari Bingwa kutoka maeneo mbalimbali ili watoe huduma kwa wananchi kila mwaka.

Toka zoezi la Madaktari Bingwa waanze kutoa huduma mbalimbali za matibabu wilayani Urambo wameshafanya oporesheni 750  na wamefanikiwa kuwaona wagonjwa 8,339

Mwisho.


 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here