Home LOCAL RAIS SAMIA: MICHEZO INAKUZA JINA LA NCHI YETU

RAIS SAMIA: MICHEZO INAKUZA JINA LA NCHI YETU

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi Mratibu wa Kifimbo cha Malkia (Queen’s Baton Relay) hapa nchini Bw. Hanry Tandau, kama ishara ya uzinduzi wa michezo ya Jumuiya ya Madola, wakati kilipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Novemba, 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (African Development Bank Group – AfDB) Dkt. Akinwumi A. Adesina leo tarehe 13 Novemba, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mara baada ya kupokea Kifimbo cha Malkia (Queen’s Baton Relay) chenye ishara ya uzinduzi wa michezo ya Jumuiya ya Madola, wakati kifimbo hicho kilipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Novemba, 2021.
 
Na. Paschal Dotto-MAELEZO

Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kuhakikisha maandalizi ya kushiriki Mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika mwaka 2022, Jijini  Birmigham Nchini Uingereza yakamilike mapema kwa kuchagua wanamichezo wenye weledi na ushindani mkubwa.

Akizungumza katika Hafla ya Mapokezi ya Kifimbo cha Malkia Yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema kuwa michezo inaleta heshima na kukuza jina la Tanzania kwani ushiriki wa Watanzania katika Michezo hiyo  umekuwa ukionekana vizuri.

“Katika Michuano hii, nakumbuka kaka yetu, Titus Simba alipambana katika hali ngumu na alifanikiwa kutuletea medali ya kwanza ya dhahabu baada ya kumshinda mpinzani wake John Conte, lakini mwaka 1974 Filbert Bay pia alituheshimisha kwa kutulea medali ya dhahabu na kuitangaza nchi yetu, hii inafanya nchi yetu kujulikana duniani huko”, Rais Samia.

Rais Samia alisema kuwa vyama mbalimbali nchini vimeanza maandalizi ya kushiriki Mashindano ya Madola mwaka 2022, na hapa akaigiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kusimamia kikamilifu maandalizi hayo ili Tanzania iweze kurejesha heshima yake ya kutwaa medali katika michezo mbalimbali kama ilivyokuwa hapo awali.

Aidha, Rais Samia alieleza na kutambua ushiriki wa Tanzania katika Michezo hiyo kwani Tanzania imekuwa mshiriki mzuri ambapo mpaka sasa ina medali 21 katika michezo mbalimbali zikiwemo sita za dhahabu (6), sita za Fedha (6) na tisa za shaba (9).

“Natambua Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya madola haijawahi kurudi bila kupata medali tangu tuanze kushiriki, isipokua miaka  mitatu, 2010, 2014, 2018, hii inamaana kwamba leo siyo tu tunapokea kifimbo, lakini pia ni wakati wa kilitafakari hili, kifimbo hiki sasa iwe kama kengele tunapigiwa kinakuja kitu tujitayarishe kwa hiyo twende tukajitayarishe vizuri”, Rais Samia.

Rais Samia amewataka Watanzania kuiunga mkono timu ya taifa katika mchezo wake dhidi ya Madagascar kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, amesema Watanzania wasife moyo kwani Timu ina nafasi ya kushinda.

Pia alimpongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, TFF na Wadau wa Michezo kwa kuonyesha ari na hamasa kubwa wakati wa maandalizi ya mchezo wa Taifa Stars na Timu ya Taifa ya DRC Congo ambapo Tanzania ilipoteza mchezo huo.

Kwa upande wake Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuwa Wizara iko tayari kuhakikisha washiriki wa Michezo ya Jumuiya ya madola mwaka 2022 wanashiriki michuano hiyo vizuri.

“Nikushukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kutuheshimisha sisi wanamichezo na leo tena tuko hapa nikuhakikishie wasaidizi wako katika sekta ya michezo tayari tumeshachukua hatua za kuimarisha sekta hii ili kuweza kuwa na wachezaji mahiri wengi watakao tuwakilisha katika mashindano mbalimbali ya kimataifa yakiwemo haya  ya Jumuiya ya Madola.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here