Home LOCAL MADARASA 332 KUKAMILIKA IFIKAPO DESEMBA –RC MKIRIKITI

MADARASA 332 KUKAMILIKA IFIKAPO DESEMBA –RC MKIRIKITI


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kulia) akiwa na Katibu Tawala Mkoa Denis Bandisa wakati wa ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye Manispaa ya Sumbawanga hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akikagua mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa kwenye shule ya sekondari Chanji Manispaa ya Sumbawanga.

Maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Chanji Manispaa ya Sumbawanga.
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa kwenye shule ya sekondari Mlimani Manispaa ya Sumbawanga ambapo changamoto ya uhaba wa maji inakwamisha kasi ya ujenzi.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

 Na: Amani Kassimba, RUKWA.

Halmashauri za mkoa wa Rukwa zimetakiwa kuhakikisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule za sekondari na msingi chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 yanakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

“Maelekezo yangu ni kuwa tupo nyuma ya ratiba ya utekelezaji miradi hii hivyo nataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuongeza kasi ya usimamizi na ufuatiliaji ili fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan zipate matokeo tarajiwa kabla ya Desemba 15 madarasa yote yawe yamekamilika kujengwa” alisema Mkirikiti.

Akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya elimu na afya kwenye Halmasahauri ya Manispaa ya Sumbawanga (22 Novemba,2021) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliagiza Wakurugenzi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika pasipo visingizio kwa kuwa fedha tayari zipo kwenye akaunti zao tangu mwezi Octoba mwaka huu.

Mkirikiti aliongeza kusema, katika kutekeleza miradi hiyo ya ujenzi ni budi halmashauri zikazingatia matumizi sahihi ya fedha kwa kuwa na miradi bora na endelevu ambapo msisitizo vifaa kama saruji, mbao na mabati vinunuliwe kwa kuzingatia bei ya soko.

Aliongeza kusisitiza ushirikishwaji wa kamati za ujenzi kwa kila mradi kulingana na Mwongozo ulitolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi ambapo wananchi wanatakiwa kutambua na kushiriki kwenye miradi hii.

Kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Mkoa wa Rukwa ulipokea jumla ya shilingi 8,940,000,000 ambapo kati hizo shilingi 6,800,000,000 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 332 ya shule za sekondari na madarasa 74 kwenye vituo shikizi pamoja na mabweni ya walemavu.

“Jumla ya madarasa 259 kwa shule za sekondari yenye thamani ya shilingi 5,180,000,000, vyumba vya madarasa katika vituo shikizi vya shule za msingi 73 yenye thamani ya shilingi 1,460,000,000 na mabweni mawili kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu yenye thamani ya shilingi 160,000,000 yatajengwa kupitia mradi huu kwenye mkoa wa Rukwa” alisisitiza Mkuu wa Mkoa Mkirikiti.

 Aidha,  kiasi cha shilingi 2,140,000,000 kati Bilioni 8.940  zitatumika kwa ajili ya sekta ya afya kwa ajili ya ujenzi wa majengo (2) majengo ya huduma za dharura (EMD) kwa Milioni 600 na ujenzi jengo moja la huduma za wagonjwa mahututi (ICU) kwa shilingi Milioni 100 wilaya ya Kalambo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkoa pia utatekeleza ununuzi mashine za Mionzi tatu (3) (X-Ray) kwa shilingi Bilioni 1.26 na ujenzi wa nyumba mbili (2) za watumishi wa afya  Nkasi na Kalambo kwa shilingi Milioni 180.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Lukangao Robert Kasitu alisema changamoto ya uhaba wa maji inakwamisha kasi ya utekelezaji mradi huku Mkuu wa Shule ya ekondari Itwelele Mwakasege Peter akisema changamoto ni upatikanaji wa vifaa vya viwandani kama saruji na nondo kwa wakati.

Mwisho.

Imeandaliwa na,

Afisa Habari Mkuu

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa

SUMBAWANGA

30.11.2021

Previous articleMSTAHIKI MEYA JIJI LA ARUSHA MGENI RASMI KONGAMANO LA FURSA SEKTA YA MUZIKI
Next articleNAMTUMBO WATAKIWA KUONGEZA KASI YA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here