Home ENTERTAINMENTS JUSTDIGGIT WAMTANGAZA MSANII BEN POL KUWA BALOZI WAO

JUSTDIGGIT WAMTANGAZA MSANII BEN POL KUWA BALOZI WAO

Anaripoti: Said Mwishehe, Michuzi Blog.

SHIRIKA la Justdiggit  limesema kuwa matumizi ya njia asilia na mbadala yanaweza kupunguza ongezeko la joto duniani kwa asilimia 37 , hivyo wamedhamiria kuifanya Afrika kuwa ya kijani kibichi katika miaka 10 ijayo.

Akizungumza leo Novemba 30,2021 jijini Dar es Salaam wakati wa kutambulisha msanii wa muziki wa kizazi kipya Benard Paul Mnyang’anga a.k.a Ben Pol kuwa Balozi na Msemaji wa Justdiggit Barani Afrika kwa kushirikiana na Lead Foundation, Meneja Mawasiliano Afrika wa Shirika hilo Meron Bezabeh amesema  hadi sasa wamefufua hekari 60,000 na kupanda miti zaidi ya milioni 6.3.

“Pia tumeendelea na miradi ya uwekezaji na utunzaji mazingira kwa kupanda miti kwa kushirikiana na wabia , wakulima na jamii ikiwa pamoja na Justdiggit kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa suluhisho la mabadiliko ya tabianchi , ikiwemo ukataji miti , ukosefu wa maji na hali ya hewa inayochagizwa na shughuli za kibinadamu,”amesema Bebeh.

Akimuelezea Ben Pol, Bezabeh amesema wamevutiwa na msanii huyo kwa sababu ni mmoja ya wasanii maarufu Afrika Mashariki ambaye amekuwa mstari wa mbele katika harakati za uhamasishaji wa mazingira, hivyo kwao ni mtu sahihi anayeweza kuwa balozi na msemaji wao Barani Afrika.

“Ben Pol anajivunia kujitolea kwa nguvu na kutumia muda wake katika uhifadhi wa mazingira kama shujaa wa Umoja wa Mataifa wa malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s), aidha Ben Pol amekuwa balozi anayeheshimika wa uhifadhi wa mazingira wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sasa Balozi wa Justdiggit,”amesema.

Aidha amesema lengo la Justdiggit , Lead Foundation na Ben Pol ni kujenga na kuongeza uelewa kuhusu kufufua upya mazingira ya Afrika kuwa kijani kibichi kwa kuhamasisha upandaji miti na kushughulia suala la mabadiliko ya hali ya hewa inayoendelea kote duniani.

Pia wamelenga kuharakisha na kuongeza matokeo chanya ya ufumbuzi wa asili kwa kushirikiana na Lead Foundatio katika kutatua changamoto zauharibifu wa mazingira katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.

“Kwa kutekeleza miradi mingi ya upandaji miti Justdiggit kwa kushirikiana na Lead Foundation tumefaulu kurejesha mamilioni ya miti kwenye maeneo ya mradi tunayosimamia pamoja na kuelemisha wa kulima kuhusu njia za asili za kuweka kijani kibichi kwa kupanda miti katika mazingira haribifu,”amesema Bezabeh.

 
Kwa upande wake Ofisa Miradi wa Lead Foundation Njamasi Chiwanga katika kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu utunzaji wa mazingira, wamekuwa wakitoa elimu kwa baadhi ya wakulima huku akielezea mradi wa upandaji miti wanaoendelea nao katika Mkoa wa Dodoma ambapo hadi sasa wameshapanda miti milioni 6.3 na malengo yao ni kupanda miti mililioni nane ifikapo mwaka 2022.

Ameongeza katika Mkoa wa Dodoma wamepiga hatua na tayari mradi huo wa kupanda miti umeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Singida huku akitumia nafasi hiyo kuelezea kuwa imekuwa rahisi kumtumia Ben Pol kwasababu uhifadhi wa mazingira ni jambo ambalo lipo kwenye moyo wake na amekuwa akijitolea bila kulipwa fedha.“Pia msanii huyo ametunga nyimbi mbalimbali za kuhamasisha utunzaji wa mazingira lakini kubwa zaidi anatoka Dodoma, kwa hiyo tunafurahia kufanya naye kazi kama mtoto wa nyumbani.”

Wakati Ben Pol yeye amesema anashukuru kuteuliwa kuwa balozi na msemaji wa Justidiggit kwa kushirikiana na Lead Foundation na kuahidi atakuwa balozi mzuri katika kutoa elimu na kuihamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira kama hatua mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Jukumu la kutunza mazingira ni la kila mmoja wetu, mimi nimetumika tu kama alama lakini niwajibu wetu sote.Najivunia kuwa mwanaharakati wa mazingira wa kujitegemea lakini pia ni Balozi wa Mazingira wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais -Mazingira na wakati huo huo nikiwa Shujaa wa Umoja wa Mataifa katika utunzaji wa mazingira,”amesema.

Ameongeza atatumia sanaa yake ya uimbaji na mitandao yake ya kijamii katika  kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu utuzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano Mshauri wa Kampuni ya Kifaransa ya Bollor’e Trasport& Logistics Fey Malonga ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa ushirikiano ikiwa pamoja na kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaomba vyombo vya habari muendelee kushirikiana nasi katika kuelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira, hivyo tunaomba msiishie hapa, tumekuwa tukiandaa taarifa nyingi pamoja na dokumentari nyingi ambazo zinazungumzia umuhimu wa kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yetu, lengo letu sote kwa pamoja tusukume gurudumu hili,”amesema Malonga.

Mwisho. (Credit – Michuzi Blog).

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here