Mkurugenzi Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) Dkt. Anselm Moshi(katikati mwenye tai) akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Yebeltal Getachew Twiga Foods Limited, jijini Nairobi nchini Kenya, alipotembelea kuona na kujiridhisha uwezo wa kampuni hiyo wa kuhifadhi na kusambaza nafaka kabla ya kuingia mkataba wa uuzaji mazao ya Bodi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt. Anselm Mungu akipena mkono na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Twiga Foods Limited.
Makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya katika soko la nafaka kati ya Kenya na Tanzania ili kuleta tija kwa wakulima na wazalishaji wa nafaka hasa kwa Tanzania ambao wanazalisha kwa wingi kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Twiga Foods Limited ya Kenya Bw.Yabeltal Getachew Dkt. Moshi amesema, Bodi ya mazao Mchanganyiko Tanzania imeendelea kupanua wigo wa masoko kwa kufanya kazi na wafanyabiashara mbalimbali katika ukanda wa Afrika mashariki ili kujenga soko imara kwa wazalishaji wa mazao ya nafaka nchini.
“Nimefanya ziara hii ya kikazi jijinini Nairobi nchini Kenya katika jitihada za kupanua masoko ya mazao ya wakulima wetu kule Tanzania na lengo la kutembelea kampuni ya Twiga Foods Limited ni kufanya mazungumzo nao na kujenga msingi wa kibiashara kati ya nchi zetu mbili ili wakulima wetu wasihangaike kutafuta masoko ya kuuza mazao yao,” Amesema Dkt.Moshi.
Ameongeza kwamba, wamekwenda nchini Kenya kwa mwaliko wa Kampuni ya Twiga Foods Limited ili kuona miundombinu waliyokuwa nayo kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nafaka ambazo zinazalishwa na Bodi ya Mazao mchanganyiko nchini Tanzania, anbapo kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu lakini hatimaye umefika wakati wa kusaini mkataba wa ushirikiano.
Aidha, Dkt. Moshi amefafanua kuwa kampuni hiyo inayo miundombinu ya kisasa kabisa ya kupokea kuhifadhi na kusambaza nafaka, zikiwemo Roboti mbalimbali, jambo ambalo limetuvutia kufanya nao kazi tukiamini kwamba kutakuwa na ufanisi mkubwa katika ushirikiano huu.
Amesema, Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha nafaka na mazao mengine ya Mikunde, Mtama,mazao ya Mbogamboga, Mazao ya Matunda na Maua hivyo ameahidi kwamba watafanya nao kazi kwa manufaa ya nchi zote mbili.
“Jambo kubwa ambalo wao wamelieleza ni kumfikishia mlaji chakula kwa bei nafuu zaidi na kwa mtazamo wetu hili ni jambo muhimu sana kwamba mlaji aweze kupata chakula kwa bei nafuu na kiasi kingine cha fedha zake akitumie katika shughuli za maendeleo,” Amesema Dkt.Moshi
Dkt. Moshi amefafanua kuwa katika nchi zetu hizi za Kiafrika uzalishaji wa chakula unafanywa na wakulima wadogowadogo hivyo kuna haja ya kuwekeza kwa wakulima wadogo ili kuwasaidia waweze kujikwamua kiuchumi, kwa kuwaunganisha pamoja katika vikundi, au vyama vya ushirika waweze kuzalisha kwa tija na kupata mazao mengi, lakini pia kuuza kwa bei nafuu, ambapo kwa Tanzania limewezekana kwa kiasi kikubwa.
“Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko tutashirikiana na wenzetu ambao tayari wao wanamtandao mkubwa wa masoko ili kuwaunganisha wakulima wetu na kuingia nao mikataba ambayo itawawezesha kuuza mazao yao bila tatizo mara baada ya kuzalisha.” Amemaliza Dkt. Moshi