Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza kwenye Warsha juu ya Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi iliyoandaliwa na HakiRasilimali katika wiki ya Azaki 2021, iliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kwanza- kulia) akimsikiliza Waziri wa Madini, Doto Biteko (Pili-kulia) wakati akizungumza kwenye Warsha juu ya Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi iliyoandaliwa na HakiRasilimali katika wiki ya Azaki 2021, iliyofanyika jijini Dodoma, Oktoba 25,2021. Wa Tatu kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.
Wadau mbalimbali wakisikiliza mada mbalimbali ambazo zilikuwa zikitolewa kwenye Warsha juu ya Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi iliyoandaliwa na HakiRasilimali katika wiki ya Azaki 2021, iliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akisikiliza mada mbalimbali ambazo zilikuwa zikitolewa kwenye Warsha juu ya Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi iliyoandaliwa na HakiRasilimali katika wiki ya Azaki 2021, iliyofanyika jijini Dodoma.
DODOMA.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa na Wizara ya Nishati inawanufaisha watanzania wote kwa ujumla.
Aliyasema hayo, Oktoba 25,2021,kwenye Warsha juu ya Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi iliyoandaliwa na HakiRasilimali katika wiki ya Azaki 2021, inayoendelea jijini Dodoma.
Wakili Byabato, aliitaja baadhi ya miradi hiyo ni Mradi wa Kuchakata na kusindika gesi Asilia (LNG) na mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki( EACOP) ambapo ameeleza kuwa miradi hiyo ipo katika hatua za utekelezwaji wake.
Alisema, Wizara imelielekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ipite katika mikoa yote Nane ambayo bomba la mafuta linapita na kubaini fursa mbalimbali ambazo zinapatikana katika mikoa husika ili watanzania wazijue na waweze kunufaika nazo.
“Serikali ya Awamu ya Sita imetoa maelekezo mahsusi kabisa kuwa kila Mtanzania anufaike na ashiriki katika miradi hii na sisi Wizara ya Nishati tumeshaweka utaratibu kwa upande wa bomba la mafuta TPDC itaenda kwenye Mikoa yote kuangalia kwa namna gani fursa zilizopo katika maeneo hayo zitawanufaisha Watanzania,” alisema
Kwa upande wa mradi wa Gesi, Wakili Byabato alieleza kuwa Wizara ya Nishati inatambua kuwa jukumu la kuhakikisha mradi wa Gesi wa LNG unaanza mara moja na kwa kuzingatia hilo Majadiliano baina ya timu ya majadiliano ya Serikali na wawekezaji ya mradi huo itaanza kazi rasmi Novemba 8, 2021.
Aidha, alieleza kuwa mradi huo utakapokamilika utakuwa na manufaa mengi kwa Taifa kwa ujumla wake, ambapo gesi nyingi itapatikana ambayo itatosheleza kwa matumizi ya ndani na pia itaweza kuuzwa nje ya nchi ambapo nchi itaweza kujiongezea pato la Taifa.
Sambamba na hilo, alisema kuwa Watanzania wanaendelea kunufaika na matumzi ya Gesi majumbani na kwenye viwanda ambapo alieleza kuwa wananchi wengi wa Mkoa wa Mtwara walinufaika na gesi hiyo.
Alieleza kuwa, huo ni mkakati endelevu wa kusambaza gesi majumbani na Serikali itahakikisha kwamba inafika kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisitiza kuwa miradi hiyo ambayo inatekelezwa na Wizara ya Nishati ishirikishe watanzania walio wengi na amewaasa watanzania kuendelea kuzalisha bidhaa ambazo zitaweza kununuliwa katika miradi hiyo.