Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Wanawake nchini Urusi ambapo Rais wa ncbi hiyo Vladimir Putin alihutubia Kongamano hilo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima akizungumza na wataalam wake mara baada ya ufunguzi wa Kongamano la Wanawake nchini Urusi ambapo Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin alihutubia Kongamano hilo.
Picha zote na KItengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Na: WAMJW-St. Petersburg, URUSI
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonesha kuwa wanawake ni muhimu katika maendeleo ya taifa lolote kulingana na asili ya majukumu yao wanayoyafanya hasa katika malezi kwa mtoto.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mara baada ya kushiriki kwenye Kongamano la tatu la Wanawake lililofunguliwa na Rais huyo na kuhudhuriwa viongozi wa mataifa mbalimbali nchini hapa.
Dkt. Gwajima amesema kuwa Rais huyo amebainisha kwamba ni namna gani wanawake ni muhimu katika hatua za awali za malezi na makuzi ya mtoto ambapo mambo mengi ya msingi ambayo mtoto anapaswa kupatiwa katika msingi wa makuzi yake mwanamke anahusika moja kwa moja kwani muda mwingi anakuwa na mtoto katika malezi yake.
Rais Putin amerejea mfano wa taifa la Urusi ambalo linafanya vizuri katika kuwapa nafasi Wanawake waweze kushiriki kwenye maendeleo ya nchi na jinsi gani Wanawake wanapewa fursa katika nyanja zote za maendeleo la taifa kwa sekta zote.
“Tumeweza kujifunza kwamba hata sisi nyumbani muelekeo anaochukua Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wa kuwajenga na kuwawezesha wanawake katika nyanja zote wasiachwe nyuma ni muelekeo sahihi kwani imejionesha katika nchi kubwa kimaendeleo duniani ziliweza kuona msingi mzima wa nafasi ya mwanamke katika kuchangia maendeleo ya jamii”
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa wanawake ndio wanaoleta Taifa kuwa na sura fulani na tabia nyingi wanazorithi watoto wetu wakiwa wadogo zinabaki katika kumbukumbu zao na ndizo zinazojenga taifa mbele ya safari.
Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Rais Putin amewapa changamoto hivyo wanaporudi Tanzania lazima wakafanyie kazi kwa nguvu ili dhamira ya Mhe. Rais Samia ya kuwatoa wanawake wengi ambao wapo nyuma na hawana nafasi nzuri kimaendeleo wapande juu na wachangie maendeleo ya taifa.
Hata hivyo Dkt. Gwajima ameahidi kutokana na Kongamano hilo Serikali ya Tanzania itajipanga kuwa na kongamano la Wanawake kupitia Majukuwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambayo yapo kwenye ngazi za halmashauri hadi Mikoa ili kuweza kujiandaa kwa miaka inayokuja kuwasilisha yatokanayo na kongamano hili na hata kuwaalika mwanawake wa mataifa mengine wafike Tanzania na kuona mafanikio yatakayofikiwa na wanawake wa Tanzania.
Wakati huo huo akizungumza na Kituo cha Runinga cha Serikali cha “Russia One” Dkt.Gwajima alibainisha kuwa Tanzania ipo salama kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 na kwamba idadi ya maambukizi yamepungua huku akitolea mfano kati ya tarehe 2 hadi 8 mwezi Oktoba Tanzania iliandikisha kesi mpya 77 na wagonjwa 171 ndio waliokuwa wamelazwa ukilinganisha na idadi ya watu waliopo na hivyo kuwaondoa hofu wananchi wa Urusi na kuwathibitishia mipaka ya Tanzania ipo wazi hivyo hamna haja ya kufungia ndege zao kuruka Tanzania na za Tanzania kuruka Urusi.
Kwa upande wa utalii Waziri huyo aliwathibitishia Urusi kuwa Tanzania inapokea idadi kubwa ya watalii kutoka mataifa mbalimbani na kwamba idadi ya watalii kuanzia Mwezi Agosti 2020 hadi Februari, 2021 zaidi ya watalii laki moja (100,000) waliweza kuingia Tanzania na waliondoka wakiwa salama.
Akielezea kuhusu Madini Dkt. Gwajima alisema Tanzania ndio nchi Pekee duniani inayozalisha inayozalisha madini ya Tanzanite na ni moja ya vito adimu na yenye thamani ambayo huchimbwa kaskazini mwa nchi katika eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara hivyo amewaalika wawekezaji kutoka nchini Urusi kuwekeza katika Sekta hiyo hususan kwenye Masuala ya uongezaji thamani wa madini hayo.