Selemani Bishagazi kiongozi wa kikukundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni ambacho waanzilishi wake ni washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (TGNP) maarufu kama GDSS.
Na: Mwandishi wetu, DODOMA.
Wadau mbalimbali wametoa maoni yao juu ya mpango wa mashirika yanayotoa ufadhili kwa taasisi na vikundi vya kijamii nchini kuiga mfano wa shirika la Women fund trust (WFT) linalotoa ruzuku kuunga mkono kazi mbalimbali zinazofanywa na vikundi vya kijamii pamoja na mashirika yanayofanayakazi ya kutetea haki za wanawake na wasichana hapa nchini.
Akiwasilisha Mada kwenye kilele cha Wiki ya Azaki iliyomalizika rasmi Octoba 28 Jijini Dodoma, Mwanaharakati wa masuala ya jinsia Selemanni Bishagazi ameeleza namna Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ilivyosaidia kujenga uelewa ndani ya jamii kupitia vituo vya Taarifa na Maarifa kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo kwa sasa kuna mafanikio makubwa yaliyotokana na harakati hizo nakwamba tayari kuna baadhi ya halmashauri zimeanza kutenga bajeti yenye mrengo wa kijinsia ikiwemo halmashauri ya Mbeya.
Akizungumzia kuhusu Shirika la Women fund trust (WFT), Bishagazi amesema kuwa Shirika hilo limekuwa likitoka ruzuku hadi kwenye vikundi vya kijamii kwa lengo la kusaidia jitihada mbalimbali zinazofanywa na vikundi hivyo katika kuleta mtazamo chanya na kuwaletea maendeleo.
“Wanachoangalia WFT kwa vikundi ni namna gani kikundi kina uwezo wa kuendeleza Tapo la ukombozi wa mwanamke na mtoto wa kike ili kumsaidia kuweza kujitambua na kujisimamia katika kujiletea maendeleo yake na jamii inayomzunguka” amesema Bishagazi
Akitoa mfano wa kikundi cha Sauti ya jamii Kipunguni cha Jijini Dar es Salaam, amesema kuwa awali hawakuwa na uelewa hata wa kuandika mradi lakini walipata msaada wa wataalamu kutoka Women Fund Trust kwa kutambua thamani ya kazi wanayoifanya.
“Kwakweli Women Fund Trust wenyewe wanaangalia kazi mambo mengine baadae, wanathamini sana kazi, tunashukuru sana” ameongeza.
Ameshauri Mashirika kutoangalia makaratasi na elimu za watu ndio watoe misaada nakwamba yaendelee kuamini kuwa mabadiliko ya kuondoa mfumo Dume yataletwa na jamii husika.
“Ikiwezekana kiwepo kipengele cha udhamini, Shirika dogo au kikundi kidhaminiwe na Afisa maendeleo au Shirika kubwa linalowafahamu, pia pale ambapo vikundi vya kijamii vinaonekana havina uwezo kama usimamizi wa fedha au namna ya kuandika miradi basi Mashirika hayo makubwa yawapatie elimu” ameshauri Bishagazi huku akiyasihi Mashirika kuwajengea uwezo wanajamii ili waweze kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao.
Bishagazi ni kiongozi wa kikukundi cha Sauti ya jamii kipunguni ambacho waanzilishi wake ni washiriki wa semina za jinsia na maendeleo (TGNP) maarufu kama GDSS, kikundi hiki kimesaidia sana kuleta mabadiliko ndani ya jamii ikiwemo kueneza uelelewa wa haki za wanawake na wasichana na kuifanya jamii kumthamini mwanamke na mtoto wa kike pia imewahamasisha wanaume na vijana kushiriki Tapo la ukombozi wa mwanamke ikiwemo kuanzisha Klabu ya kupinga ukatili ndani ya jamii.
Ametaja mafanikio mengine waliyopata kuwa ni mahusiano mazuri na viongozi, vyombo vya habari, kuwa na kituo cha mafunzo ya ujasiliamali kwa vitendo, kuanzisha vikundi vya kijamii (vituo vya Taarifa na Maarifa) kwenye kata za Chanika, Majohe, Kitunda, na Kivule na kuviunganisha na TGNP ambavyo kwasasa vimepata uragibishi na vinaendeleza Tapo la ukombozi wa mwanamke.
Kauli mbiu ya Kikundi cha Sauti ya jamii kipunguni ni ‘Harakati na Ujasiliamali’ ambapo wanaamini ukombozi wa mwanamke unaendana na uwezeshaji kiuchumi.
Ameshauri pia mashirika mengine kuiga mfumo kama TGNP wa Kulea vikundi vya kijamii kupitia vituo vya Taarifa na Maarifa ambapo Sauti ya jamii ni zao la mfumo huo.
Mwisho.