Home LOCAL SPIKA JOB NDUGAI AZITAKA ASASI ZA VIJANA KUSHIRIKIANA NA KAMATI ZA BUNGE.

SPIKA JOB NDUGAI AZITAKA ASASI ZA VIJANA KUSHIRIKIANA NA KAMATI ZA BUNGE.

 

DODOMA.

Spika wa Bunje la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Muheshimiwa Job Ndugai ametoa wito kwa Asasi za Kiraia zinazojishughulisha na kuwawezesha vijana kiuchumi nchini kufanya kazi na Kamati za Bunge mbalimbali kwa lengo la kuwasilisha maoni ya vijana katika kuanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayosaidia kuwawezesha vijana kiuchumi.

Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa ametoa wito huu Jumamosi Oktoba 23 2021 wakati alipotembelea Banda la Asasi ya Vijana – Africa Youth Transformation Tanzania wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Azaki yanayofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Tanzania, ambapo Spika huyo wa Bunge ndie alikuwa Mgeni Rasmi wa maonyesho hayo ya siku mbili yatakayomalizika Jumapili Oktoba 24.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapatia elimu mbalimbali kuhusu namna ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi na hatimae kutoa mchango wa maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Ndugai ambaye ndie alikuwa Mgeni Rasmi wa Maonyesho hayo kwa mwaka huu.

Hivyo basi, Ndugai amezishauri Asasi za Vijana nchini kudumisha mahusiano mazuri na Kamati za Bunge hususani zinazosimamia masuala ya vijana na uchumi ili wapate fursa ya kuwasilisha maoni mbalimbali yanayotolewa na vijana kuhusiana na namna gani Serikali kupitia Wizara husika inaweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana ikiwamo ukosefu wa ajira za kudumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana – AYT Bwana Justine Mponda amemueleza Ndugai kwamba Taasisi yake kwa kushirikiana na taasisi ingine – Open Mind Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikifanya kazi za maendeleo na Halmashauri mbalimbali nchini ikiwamo kutoa mafunzo ya ujasiriamali na matumizi bora ya fedha katika biashara.

“Tunawahamasisha vijana jinsi gani wanaweza kupata fedha za maendeleo kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri na taasisi za kifedha nchini. Pia kupitia mafunzo haya, tunazalisha wataalamu vijana katika Sekta za Biashara, Afya, Kilimo na nyingine za maendeleo,” amesema Mponda wakati alipokuwa anatoa maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na taasisi yake katika kuwawezesha vijana nchini kiuchumi.

Pia Meneja wa miradi wa AYT Ndugu Arafat Lesheve ameahidi kuendelea kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha kwa kuwapatia ujuzi, kuhamashisha ushiriki wao katika kuleta maendeleo endelevu yenye tija na utumiaji mzuri wa teknolojia na mitandao ya kijamii.

“Tunatoa pia elimu ya namna gani ya kutumia vizur hela zinazotolewa na taasisi za kifedha na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana, Kazi na Watu wenye Ulemavu kupitia Halmashauri kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi,”ameongeza Lesheve.

Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 60 ya idadi yote ya watu nchini Tanzania ni vijana ambao ni tegemeo la Taifa kwa siku za usoni.

Maonyesho ya Azaki mwaka huu yalitanguliwa na Maandamano yaliyoandaliwa na Shirika la Asasi za Kiraia nchini Tanzania (FCS) yaliyojumuisha maelfu ya wawakili kutoka Asasi za Kiraia mbalimbali zinazofanya shughuli za kimkakati kwenye Sekta mbalimbali nchini Tanzania, na wadau wengine wamaendeleo ikiwamo Jeshi la Polisi mkoani Dodoma na Wabunge.

Maandamano yalianzia katika Shule ya Sekondari ya Dodoma na kumalizika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete ambapo maonyesho ya Azaki 2021 yanafanyika ikiwa ni sehemu ya Sherehe za Wiki ya Azaki mwaka 2021 zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumatatu Oktoba 25 katika Ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma.

Mgeni Rasmi wa Sherehe za Wiki ya Azaki mwaka huu ambazo zinafanyika chini ya Kauli Mbiu “Azaki na Maendeleo” anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge Ndugai.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here