Home LOCAL SERIKALI IMESEMA INATAMBUA MCHANGO WA ASASI ZA KIRAIA KATIKA KUCHAGIZA UTAWALA WA...

SERIKALI IMESEMA INATAMBUA MCHANGO WA ASASI ZA KIRAIA KATIKA KUCHAGIZA UTAWALA WA SHERIA KWA JAMII



Kaimu Mkurugenzi Idara ya uratibu wa Sera Ofisi ya Rais TAMISEMI Enock Nyanda akiwasilisha mada kwenye mkutano ulioandaliwa na Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) uliokuwa ukizungumzia juu ya utawala wa sheria kuwa kichocheo cha kupunguza umasikini na kuleta usawa wa kijinsia ikiwa ni muendelezo wa Wiki ya AZAKI Jijini Dodoma.
 
katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wanachi kiuchumi (NEEC) Beng’i Issa akijibu swali lililohoji ni namna gani Serikali inachingia kuwainua vijana kiuchumi lililoulizwa na moja ya mshiriki wa mkutano huo.
 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) Lulu Ng’wanakilala, akielezea namna ambavyo LSF ilivyoweza kutoa msaada wa huduma za Kisheria kwa wananchi.
Muongozaji wa Mkutano huo Imelda Lulu Urrio akizungumza.
 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) Lulu Ng’wanakilala, akiwa kwenye picha ya pamoja na wazungumzaji na Baadhi ya watendaji wa LSF mara baada ya kumalizika kwa Mkutano huo.

Na: Hughes Dugilo, DODOMA.

Serikali imesesema kuwa inatambua na kuthamini mchango wa Asasi za kiraia nchini katika kuchangia maendeleo ya nchi na uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia utawala wa sheria na haki.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya uratibu wa Sera Ofisi ya Rais TAMISEMI Enock Nyanda alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mkutano ulioandaliwa na Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) uliokuwa ukizungumzia juu ya utawala wa sheria kuwa kichocheo cha kupunguza umasikini na kuleta usawa wa kijinsia uliowakutanisha  pamoja wadau mbalimbali zikiwemo Asasi za kiraia ili kupata mawazo ya pamoja kwenye suala zima la utawala wa sheria.

Amesema kuwa nguvu ya pamoja inaitajika kati ya Serikali na Asasi za Kiraia katika kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuelewa umuhimu na faida za utawala wa Sheria katika huduma mbalimbali za kijamii na Taifa kwa ujumla.

“Kimsingi Ofisi ya Rais TAMISEMI ina jukumu kubwa la kusimamia utawala wa Sheria na hii ina maana nyingi lakini inagusia suala zima la makusanyo na matumizi ya fedha pia kusimamia suala la ulinzi na usalama katika ngazi ya Serikali za mitaa ambazo ndizo nguzo kuu za uboreshaji wa huduma za kijamii ambapo Ofisi ya Rais TAMISEMI imepewa jukumu hilo kusimamia Kikatiba na Sheria” Amesema Nyanda.

Ameongeza kuwa moja ya majukumu yao kama Wizara ni pamoja na kuratibu na kusimamia shughuli za Asasi za Kiraia ili kujua Asasi ipi inafanya kitu gani na eneo gani ikiwa ni sehemu ya kuchangia jitihada za Serikali katika kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Naye katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wanachi kiuchumi (NEEC) Beng’i Issa akijibu swali lililohoji ni namna gani Serikali inachingia kuwainua vijana kiuchumi, ameeleza kuwa yapo maeneo mengi ambayo Serikali imewawezesha vijana kukua kiuchumi ikiwemo elimu mbalimbali za ujasiriamali na stadi za kazi zinazowawezesha kujiajiri wenyewe.

“Tumetengeneza mwongozo wa kufundisha ujasiriamali sasa unafundishwa kuanzia Shule za Msingi mpaka Vyuo Vikuu, hizi ni juhudi za Serikali kuwasaidia vijana waweze kutumia elimu zao kujiajiri wenyewe.

Akizungumza katika mahojiano maalumu mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) Lulu Ng’wanakilala, amesema kuwa, Shirika lao mpaka sasa limetoa msaada wa huduma za Kisheria kwa wananchi zaidi ya milioni 6 nchi nzima ambao wamefikiwa moja kwa moja na watoa huduma za kisheria waliopo kwenye mikoa yote Bara na Visiwani.

Ameongeza kuwa mafanikio makubwa ya watoa hutuma hao wa kisheria yamefikia asilimia sabini na tatu (73%) ambao kesi zao zimeshughulikiwa moja kwa moja na watoa huduma hao na kuzimaliza kabla ya kufika kwenye ngazi za juu za sheria.

“Kesi nyingi zinazokuja kwetu huwa zinasuluhishwa hata kabla hazijafika kwenye vyombo vya juu na haya ni mafanikio makubwa hata kwa Serikali kwani inapunguza mrundikano na msongamano wa kesi nyingi mahakamani lakini pia hata zile gharama za uendeshaji wa kesi zinapungua sana, wanufaika wakubwa ni wananchi wa kawaida kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha” Amesema Ng’wanakilala.

Aidha kutokana na umuhimu wa watoa huduma za kisheria katika jamii (Paralegals) Asasi za kiraia zimechangia kuwezesha Serikali kuwatambua rasmi kwa kutungiwa sheria inayowatambua kama chombo muhimu cha kuifikia jamii kwenye ngazi ya chini.

Amesema, Shirika lao limejikita kwenye upatikanaji wa haki wakiamini kuwa utawala wa sheria ni kitu muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi.

Mwisho.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here