Na: Mwandishi wetu,Musoma.
MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amepongeza Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kwa kuanza ujenzi wa eneo la abiria kupumzikia na vyoo kwenye Mwalo wa Mwigobero mjini Musoma.
Hata hivyo RC Hapi hakuafikiana na taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja wa TEMESA wa Mkoa huo, Vitalis Bilali, kwamba mpaka ujenzi huo ukamilike utagharimu jumla ya Sh Milioni 89.
“Tundu Moja la choo serikalini linajengwa kea Sh Milioni 1·2 hapa mnajenga matundu manne sawa na milioni 4.8,”alisema RC.
Akishirikiana na Fundi Mkuu wa Mradi huo, Mhandisi Joseph Elias, Hapi alifanya hesabu za haraka na kubaini kuwa gharama iliyotajwa ni kubwa ikilinganishwa na bei halisi za vifaa na ufundi.
“Ninafahamu michoro na gharama umeletewa na wakubwa zako, kawaambie wapitie upya hesabu ili gharama ipungue lakini mradi ukamilishwe kwa wakati huku mkizingatia ubora na thamani ya fedha,” amesema RC Hapi.
Agosti Mwaka huu, RC Hapi alifanya ziara kwenye mwalo huo na kubaini kukosekana kivuli kwa ajili ya abiria kusubiri usafiri pamoja na ukosefu wa huduma za vyoo.
Aliagiza muda wa mwezi mmoja kwa TEMESA kuanza ujenzi wa banda hilo na kuweka huduma zote muhimi kwa wasafiri ikiwamo za vyoo.