Home SPORTS RAIS ASIFU MAFANIKIO MAKUBWA KWENYE MICHEZO NA SANAA

RAIS ASIFU MAFANIKIO MAKUBWA KWENYE MICHEZO NA SANAA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Timu ya Mpira wa Miguu kwa wanawake (Twiga Stars) kwa kutwaa kombe la COSAFA jana Oktoba 9, 2021 baada ya kuifunga timu ya Malawi.

Mhe Rais ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2021 jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Maendeleo Kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19.

Akisoma hotuba yake wakati alipokuwa akianisha mafanikio ya Serikali yake katika kipindi cha miezi sita ambapo kwenye eneo la Sanaa na Michezo amesifu kazi nzuri inayofanyika katika kipindi hiki.

“Kipekee niwapongeze Twiga kwa kuchukua Kombe la COSAFA, na mara nyingi huwa nasema watoto wetu wa kike wanajitahidi sana. Hili ni kombe lao la tano nadhani kuleta nchini hivyo ninawaahidi kuwatambua” amefafanua Mhe. Rais

Aidha amesema timu ya Taifa ya Soka ya Vijana chini ya miaka 23 ni miongoni mwa wanamichezo walioiwakilisha vema nchi yetu ambapo pia amewataja mabondia Hassan Mwakinyo na Zulfa Macho kuwa wameipeperusha vema bendera ya nchi yetu kimataifa.

Mhe. Rais amewapongeza pia wasanii sita waliofuzu shindano la Afrika la urembo, utanashati na mitindo kwa watu wenye usikivu hafifu watakaoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo kidunia nchini Brazili Aprili mwakani.

Wasanii hao ni Khadija Kanyama, Carloyne Mwakasaka, Surath Mwanis, Russo Songoro, Rajani Ally na Joyce Denis Pia amewapongeza na wasanii wengine 6 walioingia kwenye mashindano ya AFRIMA ya wasanii nchini Marekani.

Amewataja wasanii hao kuwa ni Diamond, Ali Kiba, Mario, Nandy, Zuchu na Rosa Ree ambapo amewasihi watanzania wote kuwatia moyo na kuwaunga mkono hususan kuwapigia kura kwa wingi ili waibuke washindi katika shindano hilo.

Mhe. Rais amesisitiza kuwa Sekta ya sanaa na michezo ni miongoni mwa sekta muhimu hapa nchini zinazokuwa kwa kasi na kutoa mchango mkubwa katika uchumi na ajira ambapo amesema kwa kutambua hilo Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa ambao umetengewa kiasi cha shilingi 1.5 bilioni ambazo pia zitasaidia Timu za Taifa.

Kwa upande mwingine amesema Serikali imetenga Bajeti COSOTA kwa ajili ya kukusanya mapato ya wasanii na kwamba ifikapo mwezi Desemba mwaka huu Wasanii wataanza kulipwa mirabaha kwa ajili ya kazi zao wanazozifanya.

Akifafanua amesema Serikali imefuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye nyasi bandia ambapo pia amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Serikali kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo imeanzisha Tamasha Maalum la Michezo kwa Wanawake (Tanzanite) na kuratibu Tamasha la Afrika la urembo, utanashati na mitindo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia. Pia kuanzisha tuzo za wasanii.

Previous articleYANGA YAIPA KICHAPO JKU
Next articleRAIS SAMIA AZINDUA KAMPENI YA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here