Na: Mwandishi wetu,DSM
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya
amesema, anatamani kuona kipindi cha kwanza cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anafungua migodi mipya mikubwa mitatu ili kuongeza Pato la Taifa kutokana na shughuli za madini.
Aidha amewaelekeza, wafanyabiashara wa madini nchini kuwa waadilifu na waaminifu katika biashara ya madini huku akiwataka wageni na wazawa kuacha tabia ya kulaghaiana kibiashara nje ya soko na badala yake wafanye biashara kwenye masoko ya madini chini ya usimamizi wa Afisa Madini.
Naibu Waziri wa Madini Prof. Manya alibainisha hayo kwenye mahojiano ya moja kwa moja katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na kituo cha runinga cha Azam.
Prof. Manya amesema Wizara ya Madini kwa sasa inachangia Pato la Nchi asilimia 6.7 hivyo kwa kufungua migodi mingine mipya kutatimiza Sera ya Wizara ifikapo 2025 mchango wa Sekta ya Madini kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa.
“Tarajio langu ni kwamba, katika kipindi cha kwanza cha Rais Samia Suluhu Hassan kabla ya 2025 afungue migodi mingine mipya, tunatarajia kufungua mgodi mwingine pale Sengerema-Nyanzaga wa Ore Corp, tunategemea ndani ya miaka hii miwili Graphite na mradi ule wa Songwe wa Rare Earth nayo tuifungue, hii asilimia iliyobaki 3.4 kama Wizara haitushindi ili kufikia asilimia 10 ya mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa,” amesema Manya.
Akizungumzia mipango ya Serikali katika kuiimarisha Sekta ya Madini, amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuyasimamia masoko yaliyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini na kuhakikisha madini yanayongezewa thamani nchini sambamba na kuimarisha migodi ya madini ya tanzanite ambayo unaihitaji kutangazwa kikamilifu kutokana na upekee wake na kuwekewa mfumo wa kuyadhibiti.
Pia, suala la kusafisha madini nchini, Prof. Manya amesema, mpaka sasa Tanzania kuna mashine 417 za kung’arisha madini ya vito ambapo mashine 285 zipo Arusha, 95 zipo Dar es Salaam, 24 zipo Tunduru, huku 18 zikiwa Morogoro na Dodoma lengo ni kuhamasisha mashine ziongezeke ili ajira indelee kubaki nchini.
Vile vile Prof. Manya amesema ,Mwaka 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ambapo moja ya kipengele kilichoongezwa ni pamoja na kampuni kubwa na za kati kutoa hisa huru ya asilimia 16 kwa serikali.
Amesema kuwa, kabla ya Marekebisho ya Sheria ya Mwaka 2017 muwekezaji yoyote alitakiwa kulipa Corporate Tax ya asilimia 30 na tozo ya mrabaha wa asilimia 4, lakini katika muktadha wa sasa analipa mrabaha wa asilimia 6, ada ya ukaguzi asilimia 1 na ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 ya Gloss, baada ya kufanya biashara yake pia anatakiwa kulipa Corporate Tax ya asilimia 30 na baadae kulipia asilimia 16 kama hisa huru za serikali.
Ameeleza, kila madini yana mrabaha wake madini ya ujenzi na madini ya viwandani mrabaha wake ni asilimia 3, katika upande wa madini ya vito pamoja na yale ya metali mrabaha wake ni asilimia 6.
Katika hatua nyingine, Prof. Manya amesema Jambo la kutenga maeneo ya shughuli za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo wa madini ipo katika utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi hivyo Wizara ina wajibu wa kutekeleza ilani hiyo, ili wachimbaji hao wachimbe kwa tija na pasipo kubughudhiwa.