Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha Suleman Msumi akiongea katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika mkoani Arusha
.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha Suleman Msumi amewataka baadhi ya wazazi kuacha kuwageuza watoto wao wa kike kuwa kitegauchumi cha familia kwani kitendo hicho ni sawa na kuuza utu wao badala yake wawape elimu na kuwalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Msumi aliyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Ilboru ambapo aliwataka wazazi na viongozi wa kimila kubadilika kwa kuacha mila kandamizi ikiwemo kuwaozesha watoto wa kwa lengo la kupokea mali (mahari) kwani kufanya hivyo ni kuwanyima watoto kufikia ndoto zao.
“Tuko kwenye Karne ya 21 mila na desturi kandamizi ziacheni, zimeshapitwa na wakati nyie ndio chachu ya kuleta mabadiliko na kukomesha ukatili kwa watoto wa kike msiwaozeshe Wala msiwakekete wapeni elimu itawasaidia kufikia ndoto zao,” Alisema Msumi.
Alisema kuwa ukatili unafanywa na watu wa karibu hivyo wawalinde watoto wao pamoja na kuwa na ukaribu nao ili waweze kuwaeleza mambo yote yaliyotokea siku nzima kwani watoto wanapenda marafiki.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kituo cha maendeleo ya wanawake na watoto (CWCD) mama Hindu Ally Mwambego Alisema kuwa watoto wengi wanapoteza ndoto zao kutokana na ukatili wanaotendewa ambapo kama taasisi kwa kushirikiana na walimu wamekuwa wakikimbia huku na kule kuhakikisha watoto wanapata haki zao lakini wapofika katika jamii wazazi wanawarudisha nyuma kwa kukubali kumaliza kwa mazungumzo huku mtoto akiwa ndio muadhirika.
“Rushwa imekidhiri kwenye masuala ya ukatili, kesi zipo zimefikishwa mahakamani lakini wazazi wanaenda kuomba wakafanye mazungumzo kifamilia baada ya mtuhumiwa kwenda kuwarubuni na kuwapa fedha hivyo tunaiomba watuhumiwa wanapokamatwa wasipewe dhamana hadi kesi itakapoisha na hukumu kutolewa,”Alisema mama Hindu.
Sambamba na hayo pia aliwaomba viongozi wa serikalini kushirikiana na idara ya ustawi wa jamii kufanya ziara za mara kwa mara mashuleni ili kuwaelimisha wanafunzi juu ukatili na kutolea mfano Kijiji cha Engalaoni kilichopo kata ya Mwandet ambapo bado wanaendeleza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike pamoja na kuwepo kwa jitihada nyingi zilizifanywa na serikali pamoja na mashirika mbalimbali.
Naye katibu wa wazee wa mila(Malaigwanan) Emannuel Lukumay alisema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali na tasisis mbalimbali kupinga ukatili dhidi ya watoto wa kike lakini linapokuja suala la malezi Kama vile kuwafundisha watoto nidhamu isionekane kama ni ukatili ikiwa ni pamoja kuiomba serikali kuwaangalia na watoto wa kiume katika kuwalinda na kuwajengea kwani wamesahaulika.