Na: Stella Kessy.
TIMU ya KMC FC, kesho wanatarajia kushuka dimbani dhidi ya Coastal union katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara mchezo utakaopigwa dimba la Mkwakwani jijini Tanga.
Kikosi hicho kinaingia dimbani kikiwa kimepoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Black Rhino Karatu Mkoani Arusha.
KMC FC wanakuwa ugenini katika mchezo huo, watamenyana na kikosi hicho kuhakikisha kuwa wanazisaka alama tatu dhidi ya wapinzani hao ambao katika msimu uliopita walitoka sare katika michezo yote miwili nyumbani na ugenini.
Akizungumza leo ofisa habari wa kikosi cha KMC Christina Mwagala amesema kuwa licha kikosi pamoja na benchi la ufundi wamejipanga vyema kupata ushindi katika mchezo huo.
Aliongeza kuwa kikosi hicho ambacho kipo chini ya kocha Mkuu John Simkoko pamoja na wasaidizi wake, Habibu Kondo, Hamadi Ally wameshafanya marekebisho ya makosa madogo madogo yaliyojitokeza katika mchezo uliopita na hivyo kupelekea kupoteza na kwamba katika mchezo wa kesho malengo makubwa ni kupambana ili kuhakikisha kwamba Timu inashinda.
“Tumetoka kupoteza mchezo wetu muhimu wa kwanza kabisa kwenye ligi, lakini hatujakata tamaa zaidi nikama tumepandishwa hasira, tunafahamu mchezo utakuwa mgumu, wapinzani wetu pia tunawafahamu kuwa wako vizuri, lakini haimanishi kwamba KMC tunawahofia kikubwa tunakwenda kupambana uwanjani.
“Lakini pia siku zote Timu bora huwa haipotezi mechi mara mbili, tunaamini sisi ni bora, kikosi kizima kikovizuri, hata maandalizi ambayo tumefanya jana mara baada ya kufika Jijini Tanga yalikuwa kwa ustadi mkubwa na wakuleta mafaniko ya kushinda mchezo wetu wa kesho.