Na: Paul Zahoro, Geita RS.
Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) umetiliana Saini Mkataba wa Miaka Mitano wenye Thamani ya zaidi ya Shilingi Million 270 baina yake na Mkoa wa Kagera pamoja na Kanisa la African Inland Church (AICT) wenye madhumuni ya kuimarisha huduma za Afya zitolewazo na Meli maalum kuzunguka visiwa vilivyomo kwenye ziwa Viktoria kwa upande wa Geita na Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera.
Zoezi la utiliaji saini Mkataba huo limefanyika leo Oktoba 04, 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mkoa wa Kagera na Geita, Kanisa la AICT pamoja na viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).
Ndugu Musa Chogero, Katibu Tawala Mkoa wa Geita ameushukuru Uongozi wa Mgodi kwa kushirikiana na Serikali na Kanisa katika kutoa huduma muhimu za afya kwa jamii kupitia Meli hiyo hadi kufikia hatua ya kusaini Mkataba kwa mara ya pili baada ya kuhitimisha Miaka mitano ya awali ya Utoaji huduma kwa Makundi mbalimbali hasa wanawake wakati wa kujifungua Katika ukanda wa Ziwa.
Vilevile, Katibu Tawala Mkoa amewaomba wadau wote kuendelea kutoa Msaada kupitia mradi huo wa Afya ambao unasaidia sana kuendeleza uhusiano na Uhai wa wanakagera, Geita na Mikoa yote inayozunguka ukanda wa Ziwa Victoria.