Home LOCAL ENERALI IBUGE AVIPONGEZA VYOMBO VYA HABARI MAPAMBANO DHIDI YA COVID 19 Inbox

ENERALI IBUGE AVIPONGEZA VYOMBO VYA HABARI MAPAMBANO DHIDI YA COVID 19 Inbox

 

Na: Muhidin Amri,Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amevipongeza vyombo vya habari mkoani Ruvuma kwa kutekeleza ipasavyo wajibu wake kwa umma katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Covid-19.

Brigedia Jenerali Ibuge amesema vyombo habari vimechangia kutoa elimu kwa umma kuhusu chanjo ya ugonjwa huo, hali iliyosababisha Mkoa wa Ruvuma kuongoza kitaifa kwenye utoaji chanjo kwa asilimia 148.

”Mnatoa huduma muhimu sana kwa jamii naomba muendelee hivyo kuwatumia wataalam wa afya kutoa elimu ya moja kwa moja kupitia vipindi vyenu na machapisho yenu ambayo yanatoa fursa kwa wananchi kupiga simu na kupata ufafanuzi wa maswali mbalimbali “,alisema Ibuge .

Ameviomba vyombo vya habari vyenye vipindi vya kupiga simu kutoka wananchi na kuomba inapowezekana vipindi vitolewa bila gharama hali ambayo itaonesha moja ya uzalendo wa wanahabari katika masuala makubwa ya kitaifa kama mapambano dhidi ya Covid- 19.

Katika hatua nyingine,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewapongeza waumini wa kiislam kwa maamuzi ya kujenga shule na kituo cha afya ambapo amesisitiza kuwa kwa kufanya hivyo wanaisaidia serikali kuwapatia watanzania elimu na afya.

Amesema hayo wakati akiongea na waumini wa Dini hiyo katika Msikiti wa Masjid Nuru uliopo katika Mtaa wa Litunu Manispaa ya Songea.

Amesema, serikali ya Mkoa wa Ruvuma, inawaunga mkono katika utekelezaji wa miradi hiyo,hata hivyo ametaka kuwepo na uwazi namna shughuli hizo zitavyofanyika ikiwemo kujua fedha zilizoingia na matumizi yake.

Amewataka waumini wa kiislamu na watanzania kwa ujumla, kuenzi uzalendo na uhuru wetu kwa sababu Tanzania inayo tunu ya kipekee ya upendo na utangamano ambayo imeifanya nchi kuwa na umoja na Amani kwa muda mrefu.

“Hivi vitu viwili umoja na amani tusivichulie kwa urahisi,nayasema haya kwa sababu kabla ya kutaja jina langu naanza na Brigedia Jenerali, ninatambua, nimeshajionea vita maana yake nini, nimeshashiriki, kwenye vita tuilinde amani yetu kama lulu na tunu tuliyoachiwa na Mwasisi Wetu Hayati Mwalimu Julius Nyerere’’,alisisitiza Brigedia Jenerali Ibuge.

Akizungumzia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 mkoani Ruvuma,Brigedia Jenerali Ibuge amewapongeza waislamu kwa kuzingatia tahadhari za ugonjwa huo ambapo amesema, wanafanya vizuri kwenye matumizi ya maji tiririka sambamba na kusisitiza matumizi ya barakoa.

Kwa mujibu Brigedia Jenerali Ibuge,miezi miwili iliyopita kabla ya watu kuchanja hali ya corona mkoani Ruvuma ilikuwa mbaya sana, ambapo hivi sasa baada ya watu kuchanja hakuna mgonjwa hata mmoja anayetumia mashine ya kupumulia.

“Idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutokana na kupumua imepungua mno,hali hiyo imetokana na mwamko wa kuchanja,hivyo tuendelea kuhamasishana kuchanja chanjo inayokuja ya sinofam’’,alisisitiza.


Ametoa rai kwa waislam na watanzania wote kwa ujumla kujitokeza katika sensa ya watu na makazi ambayo inatarajia kufanyika Agosti 2022.

Kwa upande wake,Katibu wa Baraza Kuu la Waislam Mkoa wa Ruvuma Ustaadh Rajabu Songambele amesema, Masjid Nur katika Manispaa ya Songea imetenga hekari 80 kwa ajili ya kujenga shule ambayo itatoa elimu kuanzia chekechea hadi sekondari.

“Masjid Nur imekusudia kuwekeza kwenye elimu ili watoto wetu wapate elimu bora na kuwa katika misingi na maadili mema kwa sababu jamii hivi sasa imepoteza maadili’’,alisisitiza Ustaadh Songambele.

Katika hatua nyingine Katibu huyo wa BAKWATA amesema licha ya elimu,Masjid Nur pia imekusudia ujenzi wa kituo cha afya ndani ya Manispaa ya Songea.
MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here