Home BUSINESS BENKI YA NMB YATANGAZA NEEMA YA MIKOPO KWA WAKULIMA MKOANI ...

BENKI YA NMB YATANGAZA NEEMA YA MIKOPO KWA WAKULIMA MKOANI RUVUMA

Afisa Uhusiano wa Benki ya NMB Tawi la Songea Baraka Mwabulesi kulia akiongea na baadhi ya wateja waliotembelea banda la Benki hiyo katika maonyesho ya wiki ya mbolea Tanzania yanayofanyika katika uwanja wa majimaji mjini Songea.

Na Muhidin Amri,SONGEA


WAKULIMA  mkoani Ruvuma, wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo ya kilimo inayotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo ili kuleta tija na kukuza uchumi wao.

Hayo yamesemwa jana na  Afisa Uhusiano wa Benki ya NMB Tawi la Songea Baraka Mwabulesi, wakati akiongea na wananchi waliotembelea banda la Benki  hiyo kwa ajili ya kupata elimu ya mikopo katika maenyesho ya wiki  ya mbolea nchini yanayofanyika katika uwanja wa maji maji mjini Songea.

Amesema kuwa,lengo la NMB kutenga fedha  kwa ajili ya mikopo ni kuwawezesha wakulima  wanaofanya kilimo kama biashara kupata mitaji na kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani, sambamba na kukuza kipato chao.

Amesema, mwaka jana NMB imetoa zaidi ya  Sh.bilioni 2 kwa wakulima wa mahindi katika wilaya ya Songea ambapo kiwango cha mkopo inayotolewa ni kuanzia Sh.500,000 na kuendelea kutegemeana na shughuli za kilimo kwa mteja, na kuwataka wakulima kufika kwa wingi NMB kupata mikopo hiyo.

Amesema, kila mwaka Benki ya NMB  inatenga fedha kama mikopo yenye  masharti na riba  nafuu kwa ajili ya  kusaidia shughuli za kilimo,uvuvi,ufugaji na uzalishaji wa mazao  ili kuwawezesha wakopaji mitaji na wafanye zao kisasa na kwa tija.

“sisi NMB kila mwaka uwa tunatoa mikopo ya fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo, na mwaka huu tumetenga zaidi ya Sh.bilioni 100 kati ya hizo nyingine zimeletwa mkoa wa Ruvuma ambazo zitakopeshwa kwa wakulima”amesema Baraka.

Amehaidi kuwa, NMB itaendelea kushirikiana na wakulima katika kuhakikisha wanapata mitaji itakayowezesha kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao, na  kuchochea maendeleo kwa wakulima.

Aidha amesema, NMB itaendelea kufanya kazi ili kuhakikisha malengo ya Serikali yanafanikiwa ikiwemo kuboresha maisha ya wakulima kupitia mikopo hiyo inayotolewa katika matawi yote hapa nchini.

Baadhi ya wakulima wameipongeza Benki hiyo kwa kazi nzuri inayofanya kuhakikisha wakulima wanafikiwa na huduma za kifedha na kuwawezesha wakulima kupiga hatua za kimaendeleo kupitia sekta ya kilimo.

Hadija Abdala amesema,uwekezaji wa unaofanywa na Benki ya NMB utakuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kupanda kwa bei ya pembejeo za kilimo hasa mbolea.

Hata hivyo,ameiomba NMB kuhakikisha mchakato wa kupata mikopo inafanyika haraka ili wakulima waweze kufanya maandalizi na kuwahi msimu mpya wa kilimo.
MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here