Home LOCAL WIZARA YA AFYA YAREJESHA USIMAMIZI WA UJENZI WA MIRADI YA HOSPITALI ZA...

WIZARA YA AFYA YAREJESHA USIMAMIZI WA UJENZI WA MIRADI YA HOSPITALI ZA MIKOA KWA KATIBU TAWALA WA MIKOA.

NA: WAMJW- DOM. 

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imerejesha usimamizi wa ujenzi wa miradi ya Hospitali za Rufaa za mikoa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ili kuongeza ufanisi zaidi kutokana na Mkoa kuwa karibu zaidi na Hospitali hizo.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara kuu ya Afya Prof. Abel Makubi wakati akiongea na Waandishi wa habari Jijini Dodoma. 

“Kutokana na umuhimu wa kuzishirikisha Ofisi za Wakuu wa Mikoa katika utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa jamii, kuanzia sasa,Wizara inarejesha jukumu la usimamizi wa utekelezaji wa miradi mingine ya Mikoa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa husika ambapo miradi ya aina hiyo inayoendelea kutekelezwa,”amesema Prof. Makubi. 

Aliendelea kusema kuwa, Wizara itasaini makubaliano ya usimamizi wa Hospitali hizo na Makatibu Tawala wa mikoa (MoU) kama inavyofanyika katika Mkoa wa Katavi ili kubainisha majukumu ya Usimamizi yatakayoyafanywa ya kila upande. lengo likiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi hiyo ili ianze kutoa huduma. 

Alisema kuwa, Wizara (Afya) itahusika na kufuatilia upatikanaji wa fedha kutoka vyanzo mbalimbali na pindi fedha zitakapopatikana zitahamishiwa hazina ndogo mkoani Katavi kwa ajili ya taratibu wa malipo ili hatua za umaliziaji wa Hospitali hiyo uendelee.

Katibu Tawala Mkoa wa Katavi ataunda Kamati zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi kwa ngazi zote ambazo kamati hizo ni Kamati ya ujenzi, Kamati ya Manunuzi, Kamati ya Ukaguzi na Mapokezi, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Utunzaji wa Vifaa na Kamati ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa Mradi, alisisitiza 

Hata hivyo Prof. Makubi ameweka wazi kuwa, fedha za utekelezaji wa mradi, kiasi cha shilingi milioni 688 tayari zipo hazina ndogo mkoani Katavi ili kuwezesha ofisi ya Katibu Tawala kutoa malipo kwa ajili ya kuendeleza hatua za ujenzi zinazofuata.

Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara imeshaandaa mahitaji halisi ya Vifaa, Samani, TEHAMA na watalaamu, huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mkoa wa Katavi ili kuhakikisha kuwa maelekezo ya Mhe. Waziri Mkuu yanatekelezwa ipasavyo na Mradi huu unakamilika na kuzingatia viwango vinavyotakiwa na kwa muda mfupi.

Mbali na hayo Prof. Makubi amesema kuwa, kutokana na umuhimu wa kuzishirikisha Ofisi za Wakuu wa Mikoa katika utekelezaji wa miradi hiyo, kuanzia sasa, Wizara inarejesha jukumu la usimamizi wa utekelezaji wa miradi mingine ya Mikoa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa husika ambapo Wizara itakuwa inasaini MoU kati yake na Makatibu Tawala wa Mikoa kama inavyofanyika kwa Katavi.

Mwisho.

Previous articleBRELA YAWAHUDUMIA WANANCHI ZAIDI YA 200 NA KUTOA LESENI ZA BIASHARA PAPO KWA PAPO JIJINI DAR.
Next article“MSIWE WACHOYO WA UJUZI” – WAZIRI GWAJIMA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here