Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akitoa salamu za Wizara baada ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuzindua Upanuzi wa Kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL) tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro. Leo Septemba 23, 2021.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akihutumia baada ya kuzindua Upanuzi wa Kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL) tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro. Leo Septemba 23, 2021
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe ameeleza kuwa Viwanda vina mchango mkubwa katika ukuaji wa maendeleo kiuchumi hasa katika Sekta ya Vinywaji vikali ambavyo vina mchango mkubwa katika pato la Taifa, ajira kwa wananchi na soko muhimu kwa mazao ya kilimo yanayotumika kama malighafi katika viwanda hivyo.
Mhe. Kigahe ameeleza hayo wakati akitoa salamu za Wizara ya Viwanda na Biashara katika Maadhimisho ya Uwekezaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Ltd na Upanuzi wa Kiwanda cha bia tawi la Moshi uliofanywa na Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa, Leo Septemba 23, 2021
“Sekta ya Viwanda ni mhimili wa maendeleo katika Taifa lolote duniani kwani ni chachu ya ukuaji wa uchumi, hivyo tuko hapa Kilimanjaro kushudia mchango mkubwa wa Sekta ya Viwanda katika maendeleo ya uchumi na hasa katika Sekta ya Vinywaji vikali ambayo vina mchango mkubwa katika pato la taifa, ajira kwa wananchi wengi hasa vijana lakini pia ni soko muhimu kwa mazao ya kilimo kama malighafi, mfano katika kiwanda hiki cha Serengeti zaidi ya aslimia 85 wanatumia malighafi inayotokana na mazao ya kilimo ya hapa nchini” ameeleza Mhe. Exaud Kigahe.
Mhe. Kigahe ameleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi na bora kwa ajiri ya ufanyaji biashara na uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na hiyo inadhihilishwa na Upanuzi wa Uwekezaji katika kiwanda cha vinywaji cha Serengeti Breweries Ltd Moshi.
Aidha, Mhe. Kigahe amebainisha kuwa Kampuni ya Serengeti Breweries Ltd ina viwanda vitatu kwa mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza na Dar es salaam na imetoa ajira za kudumu zaidi ya 800 na ajira za muda zaidi ya 14,000 na Kampuni imeweza kuchangia ukuaji wa maendeleo kwa mwaka 2020 kwa kulipa kodi mbalimbali zaidi ya Bilioni 165.
Vile vile, Mhe. Kigahe ameeleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kuwatembelea, kuwasikiliza na kujadiliana na Wawekezaji ili kutatua changamoto changamoto zinazowakabili ili kuweza kuzifanyia kazi na sawa imekuwa ikifanya hivyo katika viwanda vingi, maeneo ya uwekezaji pamoja na Wafanyabiashara.