Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa akizungumza na waandishi wa habari akielezea masuala mbalimbali ya Udahili katika Ofisi za Tume hiyo Jijini Dar es Salaam. (PICHA NA: HUGHES DUGILO).
KATIBU Mtendaji wa Tume ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa leo ametoa mwenendo wa Udahili wa Awamu ya pili ya Udahili na zoezi la waombaji waliojithibitisha Udahili wa Shahada ya Kwanza katika chuo zaidi ya Kimoja katika Awamu ya kwanza ya udahili kwenye Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2021/2022, na kwamba zoezi hilo litafungwa rasmi Jumatatu Septemba 6, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Tume hiyo Jijini Dar es Salaam Prof.Kihampa amesema kuwa baada ya kukamilika kwa Awamu ya pili ya Udahili, Awamu ya Tatu ya Udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2021/2022 itaanza rasmi tarehe 18 hadi 24 septemba, 202.
“Tume inasisitiza kuwa waombaji ambao hawajatuma maombi ya udahili mpaka sasa watumie muda huu uliobaki vizuri kutuma kwa usahihi maombi yao ya Udahili kwenye vyuo wanavyovipenda”
Aidha amesema kuwa Tume inazielekeza Taasisi za Elimu ya Juu nchini kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi nakwamba waombaji wa vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa Udahili kama inavyoonekana kwenye kalenda ya Udahili iliyoko katika tivuti ya TCU.
“Mpaka sasa jumla ya waombaji 31,395 waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja kati ya 35,548 wameshajithibitisha katika chuo kimojawapo. Hivyo Tume inawahimiza wale ambao bado hawajajithibitisha wakamilishe uthibitisho wao kwa kupitia akaunti zao kwenye vyuo wanavyovipenda” ameongeza Prof. Kihampa.
Profesa Kihampa ameendelea kuwakumbusha waombaji wa Shahada ya kwanza kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.
“Kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha au kutaka kubatilisha uthibitisho wao vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa, hivyo wawasiliane na vyuo wanavyotoka kujithibitisha kupitia madawati yao na vyuo vitapokea taarifa zao na kuzifanyia kazi” Alikumbusha Prof. Kihampa.